![]() |
| Akila kiapo jana |
WAZIRI mpya wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amesema ni vigumu
kupata mwekezaji mzawa katika kazi za uchimbaji wa gesi, kwa kuwa kazi hiyo ni
gharama kubwa duniani na kampuni za uchimbaji gesi hazizidi kumi.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuapishwa kushika
wadhifa huo na Rais Jakaya Kikwete Ikulu Dar es Salaam jana, Simbachawene
alisema kauli kwamba wazawa hawawezi kuwekeza katika gesi, iliyotolewa na
aliyemtangulia, Profesa Sospeter Muhongo, haikueleweka vizuri.
Alifafanua kuwa Watanzania wanaweza kuwekeza katika nyanja ya utoaji
huduma kwa wachimbaji wa gesi na kuongeza kuwa mpaka sasa kuna maeneo ya huduma
ambayo Watanzania wangeweza kuwekeza, lakini hawajafanya hivyo.
“Kuhusu kutoa vitalu kwa Watanzania kila mtu angependa kupewa kitalu cha
gesi. Ukipata kitalu ndio umeshatoka, hata mimi ningependa kupata kimoja halafu
nikitoka nakwenda Huston (Marekani) na kukiuza na kutoka,” alisema.
Alisema la msingi ni kuhakikisha mikataba ya uchimbaji gesi, inanufaisha
Watanzania wote na katika kutoa huduma kwa wachimbaji, atapigania Watanzania
wapate fursa ya kuwekeza huko. Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na sekta
binafsi na kuongeza kuwa lakini katika ushirikiano huo, lazima kuwepo na uwiano
kati ya ushirikiano na maendeleo ya wananchi.
Kuhusu jukumu la kusambaa umeme, Simbachawene alisema atachukua Ilani ya
Uchaguzi ya CCM na kuanza nayo, ili kuhakikisha mafanikio ya usambazaji umeme
yaliyopatikana chini ya uongozi wa Profesa Muhongo, yanaendelezwa na hatimaye
Watanzania wote wapate umeme.
Naye Waziri mpya wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Lukuvi, amesema anajua Watanzania wengi wanateseka kwa kunyang’anywa ardhi
katika maeneo mbalimbali na hasa Dar es Salaam.
Amesema kwa kuwa amewahi kufanya kazi katika jiji la Dar es Salaam,
ambako alikuwa Mkuu wa Mkoa, anajua hali ya unyanyasaji katika ardhi ilivyo na
kuwataka Watanzania wenye matatizo na ardhi, kutoa taarifa ili wasaidiwe.
Lukuvi alikiri kukabiliwa na changamoto ya baadhi ya watendaji wasio
waaminifu katika sekta hiyo na kuongeza atajitahidi kukabiliana na changamoto
hiyo kwa uaminifu.CREDIT HABARI LEO



No comments:
Post a Comment