Dar es Salaam. Klabu ya Simba imethibitisha kuachana na kocha
msaidizi wa timu hiyo, Seleman Matola na kueleza kumweka hadharani
mrithi wake atakayesaidiana na kocha mkuu, Goran Kopunovic wakati wowote
kuanzia sasa.
Mapema jana, Rais wa Simba, Evance Aveva alieleza
kupokea barua ya kujiuzulu kwa Matola na kubainisha kuwa katika barua
hiyo, Matola ameeleza kutingwa na majukumu ya kifamilia hivyo hawezi
kuendelea kuinoa Simba kama kocha msaidizi.
Alipotafutwa na gazeti kuzungumzia uamuzi wake
huo, Matola alitaka aulizwe vizuri Aveva ndiye alitolee ufafanuzi suala
hilo na si yeye kwani tayari ameachana na klabu hiyo.
Hata hivyo, kocha huyo alionekana kupoteza mvuto
kwa baadhi ya mashabiki ambao mara kadhaa wamekuwa wakimshinikiza
ang’atuke Simba.
Kwa mujibu wa Aveva, Simba imepokea barua ya
kujiuzulu kwa kocha huyo juzi ikiwa ni siku moja baada ya Simba kuruhusu
kipigo cha magoli 2-1 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa.


No comments:
Post a Comment