KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

January 29, 2015

NGELEJA ANG'OKA RASMI, WENZAKE WAMMWAGIA SIFA

 Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jasson Rweikiza, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, baada ya aliyekuwa akiishikilia nafasi hiyo, William Ngeleja, kujiuzulu.
 
Ngeleja, ambaye ni Mbunge wa Sengerema (CCM), alijiuzulu nafasi hiyo, kutokana na kuhusishwa na kashfa ya kupata mgawo kutoka katika fedha zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
 
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alithibitisha jana bungeni, kuhusu Rweikiza kuchaguliwa kushika nafasi hiyo.
 
Hata hivyo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alisema jana kuwa amesikitishwa sana kumpoteza Ngeleja kama mwenyekiti wa kamati hiyo.
 
“Hii haina uhusiano na masuala yake ya Escrow na siyo utetezi wa aliyoyatenda na aliyoacha kuyatenda kuhusiana na sakata la Escrow. Ubora wake kwenye kamati siyo utetezi wa makosa yake ya Escrow,” alisema Lissu, ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo.
 
Alisema Ngeleja aliongoza kamati hiyo vizuri na kuijengea heshima kubwa tofauti na mtangulizi wake, Pindi Chana, ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
 
Lissu alisema chini ya uongozi wa Ngeleja walijadili miswada ya sheria na kupokea maoni ya wadau na kuyafanyia kazi vizuri.
 
“Na kwa sababu hiyo, quality ya taarifa za kamati iliongezeka sana hata ubora wa maoni ya wadau uliongezeka sana. Ngeleja ameiunganisha kamati kweli kweli. Wakati wa Chana kamati iliongozwa na mkono usioonekana. Kilichokuwa kimezungumzwa kwenye kamati sicho kilichokuwa kinaingizwa kwenye taarifa tofauti na wakati wa Ngeleja,” alisema Lissu.
 
Aliongeza: “Kwa hiyo, kipindi cha Ngeleja kilikuwa kizuri sana. Mimi nimesikitika sana kumpoteza Ngeleja kama mwenyekiti wa kamati.”
Wajumbe wengine waliomsifu Ngeleja, ni Ali Khamisi Seif (CUF), Rukia Kassim (CUF) na Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi).
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment