Mheshimiwa Spika,tarehe 21 Januari 2015, Kamati
ilifanya kikao cha mashauriano kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Msajili wa Hazina, Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Menejiment ya Kampuni ya Simu
Tanzania (TTCL). Lengo la kikao hicho likiwa ni kutafuta namna bora ya
kuikwamua TTCL kutoka katika hali mbaya ya kifedha na kiutendaji ili
iweze kuhimili ushindani uliopo katika sekta ya mawasiliano nchini.
Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuelezea hali ya
TTCL naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu kuwa TTCL ilianzishwa kwa
Sheria ya Kampuni ya Simu Tanzania Na. 20 ya mwaka 1993 na kusajiliwa
chini ya Sheria ya Makampuni Na. 212, tarehe 31 Desemba 1993 baada ya
kuvunjwa kwa lililokuwa Shirika la Posta na Simu Tanzania mwaka 1993.
Hadi hivi sasa Hisa za TTCL zinamilikiwa na Serikali na Bharti Airtel
Tanzania B.V kwa uwiano wa asilimia 65 na asilimia 35 sawia na hivi sasa
kuna mazungumzo kati ya Serikali na Bharti Airtel juu ya Serikali
kununua hisa asilimia 35 za Bharti Airtel ili imiliki asilimia 100 za
TTCL.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa, TTCL ilipata
hasara ya Sh. 20.883 bilioni kwa mwaka 2012 na hasara ya Sh. 16.258
bilioni kwa mwaka 2013.
Mheshimiwa Spika, kutokana na TTCL kupata hasara kwa
muda mrefu, takribani kwa miaka 10, Kampuni sasa imekuwa na jumuisho
kubwa la hasara ambayo kwa mwaka 2013 imefikia jumla la Sh. 334.48
bilioni. Ukubwa wa hasara hii umeiondolea TTCL mvuto wa kukopeshwa na
Taasisi za Fedha hata zile zenye nia ya kuikopesha.
Mheshimiwa Spika, ukosefu wa fedha za kutosha kutekeleza miradi ya Kampuni umekuwa kikwazo kwa TTCL
kukabiliana na ushindani wa kibiashara. Kwa kipindi kirefu ufanisi wa
TTCL kiuwekezaji na kifedha umeendelea kudorora. Aidha, tangu TTCL
ibinafsishwe mwaka 2001, hakuna uwekezaji mkubwa uliofanyika na mpango
wa kutafuta mkopo kutoka mabenki ya ndani na nje ya nchi unakwamishwa na
masharti ya kupata udhamini wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa fedha za kutosha
kuendesha Kampuni kumesababisha TTCL kushindwa kuboresha au kukarabati
miundombinu inayoendelea kuchakaa. Hivi sasa karibu asilimia 50 ya
miundombinu ya TTCL ni michakavu (obsolete) na inahitaji kubadilishwa na
mitambo ya kisasa.
Mheshimiwa Spika, wingi wa hasara ikijumuishwa na
uhaba wa uwekezaji umepelekea TTCL kuwa na mtaji hasi wa wanahisa
(Negative shareholders Equity) ambapo mpaka kufikia mwaka 2013 TTCL
imekuwa na mtaji hasi wa jumla ya Sh.87.896 bilioni. Hii ikitafsiriwa
kitaalamu inamaanisha kuwa TTCL ni Kampuni muflisi.
Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2005 Serikali iliipa
TTCL mkopo wa jumla ya Dola za Marekani milioni 28 kwa ajili ya kulipa
wafanyakazi waliostaafishwa, deni hilo halijalipwa mpaka sasa na
limefikiwa jumla ya Sh. 76.6 bilioni pamoja na riba. Aidha, ukiacha deni
hili TTCL inadaiwa na TCRA jumla ya Sh. 25 bilioni hivyo kufanya jumla
ya deni kuwa Sh. 101.6 bilioni.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaona kuna umuhimu wa
Serikali kufanya maamuzi ya haraka ya kuikwamua TTCL ili iweze kuendelea
kutoa huduma kwenye Sekta ya Mawasiliano ikizingatiwa kuwa Kampuni hiyo
ndiyo inayoendesha Mkongo wa Taifa, ina wafanyakazi ( 1549)
wanaotegemea ajira katika Kampuni hiyo na inatoa huduma ya internet kwa
makampuni mengine ya simu nchini.
No comments:
Post a Comment