![]() |
| Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe. PICHA|MAKTABA |
Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe amesema Watanzania wamepoteza imani na Jeshi la Polisi na ameliagiza kujitathmini na kutoa majibu kuhusu kukamatwa kwa vijana 1,200 wa kikundi cha uhalifu maarufu Panya Road.
Waziri Chikawe aliyekuwa akifungua mkutano mkuu wa
mwaka kwa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi nchini, amelitaka jeshi
hilo kujiuliza na kutoa majibu kutokana na madai kwamba baadhi ya
vijana hao wamekamatwa kwa matakwa tu ya polisi.
Alisema kuwa anazo taarifa kuwa polisi wamejikita
zaidi katika makusanyo, badala ya kuangalia usalama wa watu na ndiyo
maana wamekuwa si watu wa kuzuia tena uhalifu kama inavyotakiwa lakini
wanasubiri matukio yafanyike.
Alitaka polisi pia watoe sababu za kwa nini
wananchi wanasema kuwa kumeibuka kitengo cha dhuluma, ambacho
wamekibatiza kuwa ‘kuingia bure na kutoka kwa hela’, jambo linalotia doa
chombo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,
Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu, alisema jeshi hilo linakabiliwa na
changamoto kubwa ikiwemo uhaba wa vifaa na mafunzo katika kipindi hiki
ambacho wizi wa mitandao unaonekana kupamba moto.
IGP Mangu alikiri kuwepo baadhi ya polisi ambao wanatumia vibaya viapo vyao na kusababisha shutuma kwa jeshi zima.
Hivi karibuni, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova alitangaza kuwakamata zaidi ya vijana 1,500 kuwa
madai ni Panya Road.MWANANCHI



No comments:
Post a Comment