Mjumbe
wa Chama cha Maalbino Tanzania, Sophia Mhando (katikati), akizungumza
kwa uchungu katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo,
kuhusu vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa pamoja na maandamano hayo ya
amani ya kwenda Ikulu. Kushoto ni Mkurugenzi wa Action on Disability
& Development (ADD), Mathew Kawongo na Ofisa Habari Mahusiano ya
Umma wa Chama cha Albino Tanzania Josephat Torner.
Ofisa
Habari Mahusiano ya Umma wa Chama cha Albino Tanzania Josephat Torner
(kushoto), akizungumza kuhusu maandamano hayo. Kulia ni Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Gabriel Aluga na Mtunza
Hazina, Abdillah Omari.
Wanahabari na watu wenye ulemavu wa ngozi Albino wakiwa kwenye mkutano huo.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
…………………………………………….
Na Dotto Mwaibale
CHAMA
cha Albino Tanzania kimeandaa maandamano ya amani nchi nzima ikiwa ni
njia mojawapo ya kulaani mauaji yanayoendelea nchini pamoja na kumlilia
Rais Jakaya Kikwete kwa kile kinachodaiwa kushindwa kutokomeza mauaji ya
albino.
Maandamano
hayo yanayotarajiwa kufanyika tarehe 2/3/2015 ambapo yataanzia ofisi
za chama hicho zilizopo Ocean road kuelekea ikulu na ikiwa ni maandamano
ya tatu kufanyika tangu mwaka 2008, kipindi amabcho mauaji ya watu
wenye ualbino yalizuka na kuenea kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Ofisa Habari
Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Josephat Torner alitoa wito kwa
wazazi na mashirika ya umma na binafsi kuwaunga mkono katika maandamano
hayo ili kutokomeza suala zima la mauaji ya maalbino yanayoendelea.
“Zaidi
ya watu 76 wameuwawa na majeruhi zaidi ya 56 na makaburi 18
kufukuliwa na watu kuachwa na ulemavu wa viungo 11 kati yao na
watoto”, Torner alisema
Torner
aliendelea kusema kuwa analiomba jeshi la polisi kutoa kibali na ulinzi
na kwamba hawapo tayari kuwa wakimbizi katika nchi yao.
Nae
Mkurugenzi wa Action on Disability & Development (ADD), Mathew
Kawongo alisema kuwa atakuwa mstari wa mbele na kushirikiana nao
kuhakikisha suala zima la kutetea haki zao.
“Aidha
Kawongo alitoa wito kuwa waandishi wa habari kuwaanika hadharani wale
wote wanaofanya vitendo hivyo vya ukatili kwa albino bila kujali
vitisho.
Pia,Sophia
Mhando mwanachama wa Umoja wa albino Tanzania aliwaomba wazazi na jamii
kwa ujumla kuwa na moyo wa huruma kwa kile kinachodaiwa baadhi yao kuwa
chanzo cha mauaji hayo, na pia watasubiri kwa muda wa miezi mitatu
mbali na hapo watakwenda Umoja wa mataifa kwa mashitaka zaidi.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com)


No comments:
Post a Comment