Mrithi wa Chifu Mkwawa, Abdul Adam Mkwawa (wa kwanza kushoto) enzi za uhai wake akiwa na machifu wasaidizi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete ametuma salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Chifu Abdu Adam
Mkwawa, ambaye aliaga dunia, Jumamosi, Februari 14, 2015 hospitalini
mjini Iringa.
Katika salamu zake kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Amina
Masenza, Jumapili, Februari 15, 2015, Rais Kikwete amesema kuwa
amesikitishwa na kushtushwa na kifo cha Chifu Mkwawa ambaye amemwelezea
kama “Chifu mnzuri, kiongozi na mtu wa watu, ambaye katika maisha yake
yote alihangaika kuenzi na kudumisha kumbukumbu za utamaduni wa Mkoa wa
Iringa, za machifu wa mkoa huo na utalii wa Iringa.”
Rais Kikwete amemweleza Mheshimiwa Masenza: “Nawapeni pole sana na
naungana nawe, familia ya marehemu na wananchi wote wa Mkoa wa Iringa
katika kuomboleza maisha ya Chifu na kiongozi ambaye tutaendelea
kumkumbuka kwa mchango wake katika kujenga na kuendeleza mahusiano
mazuri ndani ya jamii. Aidha, naungana na familia katika kumwomba
Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Abdu Adam Mkwawa. Amen.”
Wakati huo huo, kesho, Jumatatu, Februari 16, 2015, Rais Kikwete
ataungana na wananchi wa Mkoa wa Iringa katika mazishi ya Marehemu
Mkwawa.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
15 Februari, 2015


No comments:
Post a Comment