Mwenyekiti wa CCM, Rais
Jakaya Kikwete akiwapungia maelfu ya wananchi wakati akiingia katika uwanja wa
Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma jana, kuongoza kilele cha sherehe za
kuadhimisha Miaka 38 ya Kuzaliwa kwa CCM. 
MWENYEKITI
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amewaonya wanachama wa chama
hicho, kuheshimu Katiba ya chama na kufuata taratibu katika kugombea nafasi za
kuteuliwa katika uchaguzi wa mkuu ili wasije kukilaumu chama, endapo
wataenguliwa na hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao.
Amesema Katiba na taratibu za chama hicho, zinafahamika hivyo ni muhimu
kwa kila mmoja kuziheshimu, ili wasije kukilaumu chama pindi watakapoenguliwa
wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea wa nafasi mbalimbali kupitia chama
hicho.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Sherehe za
Miaka 38 ya Kuzaliwa kwa CCM, zilizofanyika Uwanja vya Majimaji, Songea mkoani
Ruvuma, ambapo alisema chama kitateua mgombea ambaye hatakuwa na shaka yoyote
kwa wWatanzania.
Aidha, alitaka wanachama kutofanya ajizi katika maslahi ya nchi pamoja
na chama kwa ujumla kwa kuteua wagombea wenye sifa katika ngazi zote,
watakaoweza kukipa ushindi chama hicho na kuwatumikia wananchi. Akizungumza kwa
hisia kali, alisema wapo wanachama wana sifa za kugombea na kuongoza, lakini
hawajijui, hivyo alitaka wanachama wenzao wengine kuwashawishi wajitokeze, kwa
kuwa suala la kujitokeza sio dhambi kama kukiuka maadili.
“Kama kuna wasiosikika na wapo, tuwashawishi wajitokeze, maana si dhambi
kujitokeza, ila ni dhambi kufanya mambo ya kukiuka maadili, tusifanye ajizi
katika mambo yenye maslahi kwa taifa,” alisema Rais Kikwete.
Alisema uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni wa kihistoria nchini, kwa sababu
ni uchaguzi wa kumchagua Rais wa awamu ya tano, huku akipendekeza rais
atakayechaguliwa awe ni kutoka CCM na mwenye uwezo wa kuongoza taifa.
Rais Kikwete alisema Watanzania wasikubali kukiuka wosia ulioachwa na
Hayati, Mwalimu Julius Nyerere wa kuwa Rais bora atatoka CCM na bila CCM imara
nchi itayumba. “Lazima tuhakikishe hatufiki huko, tusikubali kukiuka wosia huu,
laana kubwa itatufika na nchi itapata hasara kubwa kwani itayumba kama
alivyosema Mwalimu Nyerere,” alisema.
Katiba Inayopendekezwa Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, Rais Kikwete
alisema jambo hilo ni kubwa na tayari ameshatoa maagizo kwa ajili ya
kuchapishwa kwa nakala za Katiba Inayopendekezwa ili ziweze kusambazwa kwa
wingi kwa wananchi waweze kuzisoma.
Aliwataka wanachama na viongozi, kuwashawishi wananchi kujitokeza
kuipigia kura ya “Ndiyo” katiba hiyo. Alisema licha ya wapinzani kusema
wamejipanga ili katiba hiyo isipite, wananchi wajitokeze kwa wingi na
kuipitisha katiba hiyo.
“Katiba Inayopendekezwa imebeba maslahi mapana ya taifa, hatujawahi kuwa
na katiba kama hii katika historia ya nchi yetu, katiba hii imekuja na ufumbuzi
wa changamoto za Muungano, hivyo hata Zanzibar wataweza kufanya mambo yao kwa
uhuru,” alisema.
Rais Kikwete alisema, haoni sababu ya kuikataa Katiba Inayopendekezwa na
aliwatahadharisha Watanzania kuwa wakikataa Katiba hiyo, itaendelea kutumika ya
sasa. “Mkikataa, hii iliyopo itaendelea kutumika mpaka miaka ijayo, Rais ajaye
hatujui kama ni atakayefuata baada ya yangu au baada ya huyo, awe na hamu ya
kuanzisha mchakato wa Katiba, mimi nilikuwa na hamu hiyo, sasa atakayekuja
anaweza akasema hilo sio kipaumbele chake,” alisema.



No comments:
Post a Comment