Kocha
Jackson Mayanja wa Kagera Sugar amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa
mechi tatu kwa kutoa lugha ya kashfa kwa maneno na vitendo kwa waamuzi wa mechi
yao na Mtibwa Sugar kuwa walipewa rushwa.
Adhabu
dhidi ya Kocha Mayanja kwenye mechi hiyo namba 136 iliyochezwa Aprili 1, 2015
kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya
40(1) ya Ligi Kuu.
Klabu
ya Mtibwa Sugar imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya timu yake kukataa
kuingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi namba 142 dhidi ya Stand
United iliyochezwa Aprili 5, 2015 katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya
14(13) ya Ligi Kuu.
Nayo
Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa mujibu wa kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu
baada ya timu yao kugoma kuingia kwenye vyumba vya kuvalia nguo (changing room)
kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati wa mechi dhidi ya Kagera
Sugar. Hatua hiyo ilisababisha wachezaji wakaguliwe kwenye gari lao.
Pia
Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kuzingatia kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu
baada ya vilevile kugoma kuingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo
hiyo namba 146 iliyochezwa Aprili 6, 2015.
Kipa
Tony Kavishe wa Polisi Morogoro amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa
mechi tatu kwa kosa la kumpiga ngumi mwamuzi msaidizi namba mbili, Hassan Zani
kwa kuzingatia kanuni ya 37(5) ya Ligi Kuu. Alifanya kosa hilo kwenye mechi
namba 147 dhidi ya Mgambo Shooting iliyochezwa Aprili 5, 2015 katika Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga.
KAMATI YA MASHINDANO TFF
Kamati ya Mashindano ya TFF ilikutana
jana kupitia maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) pamoja na taarifa ya
Ligi Daraja la Pili (SDL) iliyomalizika hivi karibuni.
Katika matukio ya SDL, Kamati imeipiga
faini ya sh. 300,000 timu ya JKT Rwamkoma ya Mara kwa kusababisha mechi yake
dhidi ya AFC ya Arusha kuvurugika. Adhabu hiyo kwa mechi hiyo iliyofanyika
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha imetolewa kwa
kuzingatia Kanuni ya 28(4) ya Ligi Daraja la Pili.
Nao makocha wa JKT Rwamkoma, Hassan
Makame na Kamara Kadede wamepigwa faini ya sh. 200,000 kila mmoja na kufungiwa
mechi sita kwa kumshambulia mwamuzi msaidizi namba moja katika mechi hiyo
iliyochezwa Machi 9, 2015.
Wachezaji Shafii Maganga, Saleh Ali,
Ismail Salim na Mussa Senyange wa JKT Rwamkoma ambao wanatuhumiwa kwa
kushambulia mwamuzi kwenye mechi hiyo suala lao linapelekwa kwenye Kamati ya
Nidhamu ya TFF kwa hatua zaidi.
VPL KUENDELEA KESHO
Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania inatarajiwa kuendelea kesho jumatano katika viwanja viwili
nchini, jijini Tanga wenyeji Maafande wa Mgambo Shooting watawakaribisha timu
ya Azam FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Mjini Morogoro
wakata miwa wa Mtibwa Sugar watakua wenyeji wa maafande wa jeshi la Magereza
nchini timu ya Tanzania Prisons kutoka Mbeya, mchezo utakaopigwa katika dimba
la Manungu Turiani.
TTF YAFUNGUA SEMINA YA WAAMUZI VIJANA
Katibu Mkuu wa
TFF Mwesigwa Selestine leo amefungua rasmi semina ya waamuzi vijana wenye umri
wa miaka 12- 17, inayofanyika katika hostel za TFF zilizopo Karume.
Akiongea na
waandishi wa habari, Mwesigwa amesema semina hiyo ya vijana imejumuisha vijana
27 kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuwaandaa kuwa waamuzi wa
kimataifa baadae.
Vijana hawa
mnaowaona hapa wanatoka katika viuto vya kufundishia waamuzi vijana nchini,
wakikua na kufuata misingi ya kazi baadae watakua waamuzi bor nchini kwa sababu
watakua wameanza tangu wadogo na kufuata maelekezo ya wakufunzi wao.
Naye Mwenyekiti
wa Kamati ya Waamuzi nchin Bw. Salum Chama akiongea na wandishi wa habari kabla
ya kumkaribisha katibu mkuu, amesema malengo yao ni kuhakikisha Tanzania inakuwa
na waamuzi wa kimataifa wengi.
Mwaka huu Tanzania
imeshika nafasi ya pili kwa kutoa waamuzi 18 wenye beji za FIFA barani Afrika,
nyuma ya Misri yenye waamuzi 22, Lengo ni kuhakikisha tunawaanda vijana wengi
waje kuwa waamuzi wa kimataifa.
Semina hiyo ya
siku 5 inatarajiwa kufungwa ijumaa tarehe
17 Mei, 2015 inajumuisha vijana kutoka mikoa ya Dar es salaam, Tanga,
Zanzibar, Mwanza, Arusha na Mbeya, kati ya vijana 37 waamuzi wawili ni
wanawake.
Wakufunzi wa
semina hiyo ni Soud Abdi, Riziki Majala na Joan Minja.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)


No comments:
Post a Comment