| Muonekano wa eneo la Ubungo-Darajani hali ilivyokuwa. |
| Wasafiri wakiwa hawajui hatma ya safari yao eneo la Ubungo. Abiria
MADEREVA wa mabasi ya mikoani na daladala wa jijini
Dar leo wamefanya mgomo kupinga agizo la Mamlaka ya Kudhibiti Usafiri wa
Majini na Nchi Kavu (Sumatra) lililowataka kwenda kusoma katika Chuo
cha Usafirishaji (NIT).
Mwandishi wetu amezunguka maeneo tofautitofauti jijini Dar na
kujionea hali halisi ya mgomo wa mabasi ya mikoani pamoja na daladala za
maeneo tofauti ya Jiji la Dar.
Mwandishi wetu pia aliweza kufika eneo la Stendi ya Ubungo na
kujionea hali ilivyokuwa asubuhi na kuzungumza na baadhi ya madereva
ambao walikuwa na kauli tofautitofati kuhusiana na mgomo huo.
Mmoja wa madereva ambaye alijitambulisha kwa jina la Ally Abdallah
Shalon anayefanya kazi zake kati ya Dar es Salaam na Dodoma, alisema
kuwa sababu kubwa ya kutokufanya shughuli zake ni kutokana na kikao
ambacho walipanga kukifanya leo kujadili agizo la Sumatra lililowataka
waende shule kusoma.
Dereva mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Khamis anayefanya
shughuli zake kati ya Mwanza na Dar es Salaam alisema sababu iliyomfanya
agome ni kupinga sheria mpya ya Sumatra iliyopitishwa na jeshi la
polisi kuwataka madereva wote wa abiria (Pasangers Services Vehicle)
kwenda kusoma kozi ya miezi miwili kwa gharama ya shilingi laki tano.
Khamisi alisema sheria hiyo inawabana sana madereva kwani moja kati
ya vipengele vya sheria hiyo imeeleza kuwa, dereva yeyote atakayekamatwa
akiwa amezidisha mwendo kasi hakuna faini yoyote bali unapelekwa
mahabusu kwa muda wa siku kumi na nne baada ya kumaliza siku hizo,
anapelekwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
“Hii sheria inatubana sana, mtu ukihitaji kubadilisha leseni yako
ikipitwa na muda unatakiwa kurudia tena kwenda kusoma darasani kwa muda
wa wiki mbili kwa ada isiyopungua laki tano na kuendelea kitu ambacho
kinatuumiza sisi madereva,” alisema Khamis.
MUSOMA
Huko Musoma, abiria zaidi 1000 waliokuwa wakisafiri kutoka Musoma kwenda Dar es Salaam kupitia mkoani Mwanza na Shinyanga na wale wa kwenda mpakani mwa Tanzania na Kenya pamoja na wa ndani ya Mkoa wa Mara wameshindwa kusafiri baada ya madareva kuitisha mgomo leo.
KIBAHA
Zaidi ya mabasi 10 kutoka mikoa ya kanda ya ziwa yamekwama huko Kibaha mkoani Pwani kutokana na mgomo wa madereva leo.
BUKOBA
Mabasi yote ya abiria yaliyotoka Bukoba Mjini leo asubuhi kuelekea Dar, Mwanza na kwingineko yamezuiliwa wilayani Muleba kutokana na mgomo wa madereva unaoendelea nchini kote. Abiria wamerudi mjini Bukoba kurudishiwa nauli zao na kuahirisha safari.
(PICHA/HABARI: DENIS MTIMA/GPL)
|


No comments:
Post a Comment