![]() |
| Rashid Charles Mberesero
Dar/Dodoma/Nairobi. Mtanzania anayedaiwa
kuhusika katika shambulizi la kigaidi lililoua watu 148 katika Chuo
Kikuu cha Garissa – Kenya, Rashid Charles Mberesero, jana alifikishwa
mahakamani na kuwekwa kizuizini kwa mwezi mmoja wakati polisi
wakiendelea kukusanya ushahidi dhidi yake.
Mtuhumiwa huyo ambaye pia anafahamika kwa jina la
Rehani Dida alirejeshwa Nairobi kutoka Garissa alikopelekwa awali kwa
ajili ya kuhojiwa baada ya kukiri kujihusisha na kundi la Al- Shabaab.
Mahakama jijini Nairobi ilisema jana kuwa
mtuhumiwa huyo ambaye hakutakiwa kujibu tuhuma hizo na wenzake wanne
watalazimika kuwa chini ya uchunguzi mkali wa polisi kwa kipindi cha
mwezi mmoja na baadaye wanaweza kusomewa mashtaka ya kuhusika katika
shambulizi hilo lililoua watu hao, wengi wao wakiwa ni wanafunzi.
Haikufahamika mara moja sababu za kuamuliwa
kuwekwa kizuizini kwa muda huo mbali ya taarifa kueleza kuwa
‘watashikiliwa na polisi tena katika kituo cha siri’.
Mwendesha Mashtaka, Daniel Karuri aliiambia
Mahakama hiyo kuwa Mtanzania huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha
tano, alikuwa amepanga safari ya kuelekea Somalia kwa ajili ya kujiunga
na makundi ya kigaidi.
Watuhumiwa hao ni kati ya 14 waliotiwa mbaroni hivi karibuni baada ya shambulizi hilo la kigaidi.
Mahakama hiyo pia imewaamuru washukiwa wengine kuendelea kushikiliwa na polisi kwa muda wa siku tano hadi 15.
Awali, Karuri aliiambia Mahakama hiyo kuwa polisi
walikuwa wakifuatilia kwa karibu uhusiano baina ya wale waliofanya
shambulizi hilo na mfanyabiashara mmoja anayemiliki hoteli mjini
Garissa. Inasemekana kuwa watu waliotekeleza shambulio hilo walikuwa
wamelala katika hoteli hiyo.
|
April 10, 2015
MTANZANIA ANAYETUHUMIWA KWA UGAIDI KENYA KIZIMBANI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment