Askari wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, H 3416 PC Charles, amejiua kwa kujipiga risasi.
Baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na kituo hicho cha polisi,
Paulo Lazaro na Furahisha Felix, walisema tukio hilo lilitokea Aprili 4,
mwaka huu, saa 1:00 usiku kituoni hapo.
“Suala hili limetushangaza, kwani sisi tulikuwa nyumbani. Ghafla
tulisikia mlio wa bunduki katika kituo cha polisi. Tulipofika, tulimkuta
askari huyo akiwa amekufa kwa kujipiga risasi,” alisema Lazaro.
Wananchi hao walisema kutokana na hali hiyo, walilazimika kuwauliza
baadhi ya askari waliokuwa zamu, ambao walidai hata wao hawajui ni
kwanini mwenzao amechukua uamuzi wa kujiua.
Waliomba ufanyike uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha kujiua
kwa askari huyo kwani inawezekana kuna kitu ambacho alikuwa amechukizwa
nacho. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda, alithibitisha
kujiua kwa askari huyo. “Ni kweli askari huyo amejiua kwa kujipiga
risasi wakati akiwa kituoni majira ya saa 1:00 usiku,” alisema Kamanda
Kaganda.
Hata hivyo, Kamanda Kaganda alisema hakuna ujumbe wowote ulioachwa
na askari huyo kuelezea sababu za kujiua. Kutokana na hali hiyo, Kamanda
Kaganda aliwataka askari wote kutatua matatizo yao kupitia kwa viongozi
wao badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha askari huyo kujiua.
CHANZO:
NIPASHE


No comments:
Post a Comment