KINAMAMA kutoka Kata ya Bukundi Wilaya ya Meatu, mkoani
Simiyu, wameandamana hadi kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Erasto Sima, kushinikiza
wapewe miili ya vijana wao wawili waliouawa na askari Mei 29, mwaka
huu.
Vijana hao Gineu Gidahasi na Gitienga Gidahasi ambao ni
ndugu wa familia moja wanadaiwa kupigwa risasi na askari wa Kampuni ya ulinzi ya
Mwiba Holding kwa madai ya kuingiza mifugo eneo pori la makao ambalo kampuni
hiyo imewekeza.
Kinamama hao walifika katika ofisi ya Mkuu huyo wa
wilaya saa mbili juzi asubuhi ambapo walilalamikia kitendo cha vijana wao
kuuawa na kisha miili yao kutoonekana na kumwomba Sima kuagiza kupatiwa miili
hiyo ili waweze kuifanyia mazishi na iwapo itashindikana watakwenda kwa Rais
Jakaya Kikwete kuomba msaada huo.
“Tumechoka na manyanyaso kutoka kwa mwekezaji huyu,
kilichotuleta hapa tunahitaji tupatiwe miili ya vijana wetu tukaifanyie mazishi
kwa heshima zote za kabila letu na iwapo utashindwa kufanya hivyo basi
tutakwenda Ikulu tumuombe Rais Kikwete atusaidie,” alisema Udamulela
Gitasori mkazi wa kijiji cha Lukale.
Walisema hadi sasa zaidi ya vijana sita wameuawa tangu
mwaka 2013 kwa madai ya kuingiza mifugo katika eneo la pori hilo ambalo
linapakana na vijiji vya Mwabagimu, Lukale na Bukundi na hivyo wamekuwa wakiishi
kama wakimbizi ndani ya nchi yao.
Naye Mbunge wa Jimbo la Meatu, Meshack Opulukwa
(Chadema), aliitupia lawama serikali kwa kushindwa kulipatia ufumbuzi suala la
wafugaji kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa mwekezaji huyo licha ya kupatiwa
taarifa na hivyo alimwomba Sima kusitisha shughuli zinazofanywa na Mwiba hadi
hapo miili hiyo itakapopatikana.
Akijibu malalamiko hayo kwa kifupi Sima alisema
serikali wilayani humo imeshaanza kulishughulikia suala hilo na tayari wote
waliohusika na mauaji hayo wameshakamatwa.
Source; Mpekuzi blog



No comments:
Post a Comment