![]() |
| Rais Jakaya Kikwete. Wakati msururu wa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotafuta ridhaa ya chama kuteuliwa kuwania urais ukifikia watu 35, Rais Jakaya Kikwete, amekana kuwa na mgombea wake na badala yake ana kura moja ya kumchagua amtakaye.
Akizungumza na Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeongoza
Kitengo cha Masuala ya Afrika Linda Thomas-Greenfield, mjini
Johannesburg mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Kikwete alisema hana
mgombea ana mpendelea kwa sababu wote ni wa kwake na wa chama chake.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, pia ilimnukuu Kikwete akisema kuwa
hana tatizo na kujitokeza kwa wagombea wengi wa nafasi ya urais zamu hii
kupitia CCM, kwa sababu hawezi kuwazuia kwa kuwa ni haki yao. Hata
hivyo, alisema kuwa wingi wa wagombea zamu hii ni jambo zuri na ni
ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka katika chama hicho na
uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10 iliyopita umekuwa
wa mafanikio.
Rais Kikwete na Linda walikuwa wanahudhuria Mkutano wa 25 wa
Kawaida wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika kwenye Kituo cha Mikutano
cha Sandton Covention Centre, Johannesburg, Afrika Kusini uliomalizika
juzi.
Hadi jana CCM ilikuwa na wanachama 35 ambao wamejitokeza kutafuta
ridhaa ya chama hicho kuteuliwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa
Oktoba 25, mwaka huu.
Waliokwisha kujitokeza hadi jana ni Makamu wa Rais, Dk. Muhamed
Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Uchukuzi, Samuel
Sitta; Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli; Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Stephen Wasira na Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk.
Titus Kamani.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi Maalum, Prof.
Mwandosya; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe; Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa
Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro.
Pia wamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu; Naibu
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia, January Makamba.
Mbali na mawaziri hao, wapo mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Makada wengine ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla; Mbunge wa
Sengerema, William Ngeleja; Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Sospeter
Muhongo; Maliki Marupu; Joseph Chagama; Makongoro Nyerere; Mwale
Malecela; Monica Mbega; Balozi Ali Karume, Balozi Amina Salum Ali na
Balozi Augustine Mahiga.
Hadi sasa walikwisha kurejesha fomu ni Sitta na Dk. Bilal, wengine wanaendelea kusaka wadhamini mikoani.
Kamati Kuu (CC) ya Chama hicho itakutana Julai 12, mwaka huu
kuwachuja wagombea na kubaki na majina matano ya kupeleka mbele ya
mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Kazi ya kuchuja ni nzito kwani miongoni mwa wajumbe wa CC kuna watia nia kama Dk. Bilal; Pinda Wasira na Dk. Migiro.
|
June 17, 2015
KIKWETE ANA MGOMBEA?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment