
Utata wa mkataba wa kiungo wa ushambuliaji wa Klabu ya Soka ya Simba, Ramadhan Singano 'Messi', dhidi ya klabu yake unatarajiwa kutolewa ufumbuzi katika kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kinachotararajiwa kufanyika kesho jijini Dar es Salaam, imefahamika.
Akizungumza na NIPASHE jana jijini, Mwenyekiti wa Chama cha
Wachezaji wa Soka Nchini (SPUTANZA), Mussa Kissoky, alisema kuwa
amepokea wito kutoka TFF na anatarajia atahudhuria katika kikao hicho
kwa ajili ya kumtetea Singano ambaye ni mwanachama wao.
Kissoky alisema kwamba wanaamini tofauti zilizopo baina ya mchezaji na klabu zitamalizwa katika kikao hicho.
"Hatima ya Messi na Simba sasa itajulikana Jumamosi, tumeitwa
katika kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, hiyo ndiyo
kamati ya juu na ambaye hataridhika na maamuzi hayo inabidi aende Fifa,"
alisema mwenyekiti huyo wa SPUTANZA.
Kamati ya Utendaji ya Simba iliyokutana hivi karibuni iliamua
kutofanya mazungumzo upya na Messi kama ilivyoagizwa na sekretarieti ya
TFF.
Badala yake Simba iliamua kuliwasilisha suala hilo katika Kamati ya
Sheria na Hadhi za Wachezaji huku ikisisitiza kwamba 'haijauchakachua'
mkataba wa nyota huyo ambaye alianzia kuitumikia klabu hiyo katika timu
ya vijana wa umri chini ya miaka 20 (Simba B).
Simba imesisitiza kwamba mkataba wa mchezaji huyo ambao ulisainiwa
chini ya uongozi uliopita wa aliyekuwa mwenyekiti, Ismail Aden Rage,
unamalizika mwakani, wakati mchezaji huyo anasema kwamba umeshamalizika.
Kufuatia tofauti hizo, Singano ameshindwa kufanya mazoezi ya pamoja
na baadhi ya nyota wa Simba ambao wameanza kujinoa kwenye gym.
KOCHA KERR KUTUA
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kwamba kocha mkuu mpya wa
timu hiyo, Muingereza, Dylan Kerr, anatarajiwa kutua nchini kati ya leo
au kesho.
Chanzo kilisema jana pia kwamba tayari mshambuliaji wa kimataifa
kutoka Kenya, Paul Kiongera, ameshawasili nchini tangu juzi na leo
ataanza mazoezi ya viungo ambayo yanasimamiwa na kocha msaidizi,
Selemani Matola.
No comments:
Post a Comment