Mgogoro wa kisiasa Zanzibar umeingia katika hatua nyingine baada ya
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kukataa hoja ya Spika wa baraza hilo ya kumwalika Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kuhudhuria kuvunjwa kwa
baraza hilo leo.
Hali hiyo inaashiria kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaiaf (SUK)
iliyoundwa na Chama cha Wananchi (CUF) na CCM baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010 imepata majaribu.
Awali akitoa taarifa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi jana,
Spika wa baraza hilo, Pandu Ameri Kificho, aliwataarifu wajumbe hao kuwa
wakati wa kuvunjwa kwa baraza hilo wageni watatu wanatarajiwa
kuhudhuria akiwamo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Makamu wa
Kwanza wa Rais Maalim Seif na mlinzi wa rais.
Hata hivyo, Kificho alisema wajumbe wa baraza hilo ndiyo wenye
mamlaka ya kukubali au kukataa wageni hao kuhudhuria na kutaka idhini
yao.
Spika huyo alipowauliza wajumbe hao kama wanakubaliana na ujio wa
wageni hao, wajumbe hao kwa kauli moja walimjibu kuwa Jaji Mkuu wa
Zanzibar na mlinzi wa Rais wa Zanzibar wanamruhusu kuingia lakini
walikataa Makamu wa Kwanza wa Rais (Maalim Seif) asiingie katika kikao
hicho.
SPIKA: Ndugu wajumbe wageni wetu wakuu kesho (leo) ni watatu na
tayari nimeshawapelekea barua ya kuwaalika kuhudhuria katika ufungaji wa
kikao hiki, nataka kauli zenu vipi bodigadi wa rais mnamruhusu?.
WAJUMBE: Ndiyooo
SPIKA: Je?, Jaji Mkuu wa Zanzibar mnamruhusu?
WAJUMBE: ndiyoooo
SPIKA: Mgeni wetu mwengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais vipi mnamruhusu?
WAJUMBE: Hatumtaki.
Spika Kificho alirudia kuuliza mara tatu swali hilo lakini majibu
ya wajumbe mara zote yalikuwa ni hayohayo ya kumkataa Maalim Seif
kuhudhuria.
Kufuatia hali hiyo, Kificho aliwaambia wajumbe hao kama hawataki
Makamu wa Kwanza wa Rais kuhudhuria kikao hicho kwa kuwa alishamwandikia
barua ya mwaliko itabidi amwandikie tena barua ya kumtaarifu kongozi
huyo kuwa asihudhurie kikao hicho kutokana na wajumbe wa baraza hilo
kukataa ujio wake.
Baadhi ya wajumbe wa CCM wakizungumza na NIPASHE, walieleza sababu za kukataa Maalim Seif kuhudhuria shughuli hiyo.
Kaimu Mnadhimu wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CCM, Ali
Salum Haji, alisema wana sababu za msingi kukataa Maalim Seif ambaye pia
ni Katibu Mkuu wa CUF kuhudhuria kikao hicho, ikiwamo kuwa yeye ni
kiongozi wa upinzani lakini wajumbe wake na mawaziri wa chama chake
wamesusia baraza hilo. CHANZO:NIPASHE



No comments:
Post a Comment