Katibu
mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Abdulrahman Kinana,
amewatahadharisha makada wa chama hicho wanaowania nafasi mbalimbali za
uongozi kuwa makini na watu wanaojiita wapambe kwani wapo kwa ajili ya
maslahi ya kifedha.
Kinana aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa ndani wa halmashauri
ya jimbo la Sumve wakati akizungumza na wajumbe wa chama hicho, wilayani
Kwimba mkoani Mwanza.
Kinana alisema kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo ni vyema
wagombea wakachukua tahadhari juu ya watu hao ambao ni wapiga debe wa
watangaza nia ili kuwawezesha kupata nafasi ya uongozi.
"Kuweni makini na hawa wajanja wanaojiita wapambe au wapiga debe,
kwa maana wapambe wengine mbali na kuujua ukweli kwamba wananchi
hawakukubali lakini bado anakula fedha zako bila kuwa na wasiwasi tena
akizidi kukupa matumaini hewa," alisema Kinana.
Alisema, maeneo mengi wagombea wameumizwa na wapambe hao hivyo ni vema kuwa makini na kuchukua tahadhali katika hilo.
Aliwasihi Watanzania kuchagua viongozi wa CCM kwani ndiyo viongozi bora wanaojua matatizo ya wananchi.
Kinana alisema kuwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,
aliwahi kusema kuwa viongozi ni wengi, lakini kiongozi bora atatokana na
Chama cha Mapinduzi.
CHANZO:
NIPASHE



No comments:
Post a Comment