![]() |
| Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba. Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye anawania uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais, ameahidi kuwa asipoteuliwa hatakuwa na kinyongo na atarejea kukijenga chama.
Aidha, ameahidi kuwa atalirudisha Jimbo la Iringa Mjini mikononi mwa CCM.
Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Mchungaji Peter Msigwa, wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kadhalika, Makamba amemwaga ahadi lukuki kwa wakazi wa mji wa
Iringa ikiwamo kuwasaidia vijana wa bodaboda, kupanua uwanja wa ndege
mkoani humo, kujenga barabara ya lami kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha
pamoja na kufufua viwanda.
Ahadi nyingine ni pamoja na kuhakikisha vijana wanaojiunga na vyuo
vikuu, wanapata mikopo bila usumbufu wowote kwa kuwa kupata elimu ni
haki yao.
Aliyasema hayo jana alipozungumza na makada wa CCM, kutoka wilaya
zote za mkoa wa Iringa, alipokuwa akitafuta wanachama wa kumdhamini.
Makamba alipata zaidi ya wadhamini 600 ambao ni zaidi ya idadi inayotakiwa na chama ambayo ni wanachama 30 kwa kila mkoa.
Aliongeza kuwa mchakato wa kumpata mgombea, hauna uhasama na kwamba
hata kama kushinda ama kushindwa atakuwa mtu wa kwanza kuanza kukijenga
chama upya ili kurudisha mshikamano.
“Mimi nitakuwa mtu wa kwanza kuanza kukijenga chama baada ya
uchaguzi mkuu, wanachama wote wanatakiwa kukaa kama familia moja ili
kujenga mshikamo pamoja na kujadili makovu ya uchaguzi,” alisema.
Makamba alisema ana imani kwamba CCM kitapitisha mgombea kwa
kujiamini bila kuogopa kusambaratika na wala wanachama wasisikilize watu
wanaojipitisha mitaani na kusema kwamba chama kitasambaratika baada ya
uchaguzi.
Kabla ya kukutana na wanachama wa CCM katika ofisi za wilaya,
Makamba alisema Iringa ni kama nyumbani kwao kwa kuwa aliwahi kuishi
hapo wakati baba yake akifanya kazi mkoani humo.
Wakati wa mapokezi yake, vijana waendesha bodaboada waliongoza
msafara wake, huku wakiimba nyimbo hadi katika ofisi za wilaya ambako
alikabidhiwa majina ya makada waliomdhamini.
|
June 12, 2015
MAKAMBA: NISIPOTEULIWA SITAKUWA NA KINYONGO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment