![]() |
| Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (53), amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Shilingi milioni moja baada ya kupatikana na hatia ya kumshambulia Mwangalizi wa Ndani wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Nassir Uronu.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro jana.
Hata hivyo, Mbowe alifanikiwa kulipa kiasi hicho cha faini na hivyo kuepuka kwenda kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.
Mbowe alikuwa akikabiliwa na kesi namba 73 ya mwaka 2011
iliyofunguliwa na Nassir; aliyedai kushambuliwa kwa kipigo akiwa katika
Zahanati ya kijiji cha Nshara kata ya Machame Kaskazini Wilaya ya Hai,
mwaka 2010.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya za Hai na
Siha, Denis Mpelembwa, alisema mahakama hiyo imemtia hatiani Mbowe kwa
kosa la kumshambulia Nassir kinyume cha kifungu cha 24 cha Kanuni ya
Adhabu, Sura ya 16 cha Sheria iliyofanyiwa Mrekebisho mwaka 2002.
“Mahakama imekuona una hatia katika kosa linalokukabili na
inakuhukumu kulipa faini ya Shilingi milioni moja au kutumikia kifungo
cha mwaka mmoja jela,” alisema Hakimu Mpelembwa.
Awali, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Issa Rajabu,
aliyekuwa akisaidiana na Wakili Albert Msando; aliiomba mahakama hiyo
kumpunguzia adhabu mteja wake (Mbowe), kwa madai kwamba ni kosa lake la
kwanza.
Kesi hiyo ya uchaguzi mkuu uliopita, imekuwa ikivuta hisia za
wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na
Tanga hasa kutokana na nguvu ya kisiasa aliyonayo Mwenyekiti huyo wa
Chadema na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Katika uchaguzi huo, Nassir alikuwa Mwangalizi wa Ndani wa Uchaguzi Mkuu akiliwakilisha Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Hata hivyo, Mbowe aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Hai kwa
tiketi ya Chadema, aliibuka mshindi kwa kupata kura 28,585, akifuatiwa
na Fuya Kimbita (CCM), kura 23,349, Hawa Kihogo (UDP) 258 na Petro
Kisimbo (TLP) kura 135.
Wakili wa Jamhuri katika kesi hiyo, Simon Feo, ambaye ni Mwendesha
Mashitaka wa Polisi, aliieleza mahakama hiyo kwamba kutokana na ukubwa
wa kosa, anaiomba mahakama impatie adhabu stahiki kwa vile makosa kama
hayo yanaharibu taswira ya jamii na hasa ikizingatiwa kuwa Mbowe ni
kiongozi wa kitaifa.
Baada ya Hakimu Mpelembwa kumaliza kusoma hukumu hiyo, Mbowe
alitolewa nje ya mahakama chini ya ulinzi mkali wa Polisi waliokuwa
wameimarisha ulinzi katika viunga vya mahakama hiyo na kumshikilia kwa
zaidi ya saa mbili; hadi alipofanikiwa kulipa faini ya Shilingi millioni
moja na kuachiwa huru.
Akiwa chini ya ulinzi wa Polisi, wanachama na wafuasi wa Chadema
waliofurika mahakamani hapo, walilazimika kujichangisha na kisha kulipia
faini hiyo kupitia Benki ya NMB na baadaye kuwasilisha mahakamani
stakabadhi yenye namba 0317489.
|
June 18, 2015
MBOWE AMALIZANA NA MAHAKAMA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment