![]() |
| Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani. "Nilirudia uanachama wangu wa CCM mwaka 2011, baada ya kustaafu
wadhifa niliokuwa nao kama Jaji Mkuu... Sina doa katika serikali au
utumishi wangu; kwa kweli hakuna Mtanzania anayeweza kuninyooshea kidole
kwa kupokea au kuhusika na vitendo vya rushwa. Kizuri chajiuza, kibaya
chajitembeza..."
Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan, ametangaza nia ya kugombea
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM), huku akieleza kuwa licha ya kuwapo kwa utitiri wa wagombea urais,
hakuna Mtanzania yeyote anayeweza kumnyooshea kidole akimtuhumu kupokea
au kuhusika na vitendo vya rushwa.
Jaji Ramadhan ambaye ni kada wa 36 kuchukua fomu ya kuomba
kuteuliwa na chama chake kuwania kiti hicho, alisema hakuna mgombea
anayemtisha kati ya wote waliomtangulia, kwa kuwa hakuna mwanajeshi
anayeogopa.
Jaji Ramadhani alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana
katika Makao Makuu ya CCM Mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kuchukua
fomu ya kuwania nafasi hiyo.
“Sina doa katika serikali au utumishi wangu; kwa kweli hakuna
Mtanzania anayeweza kuninyooshea kidole kwa kupokea au kuhusika na
vitendo vya rushwa. Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza. Mimi ni
mwanajeshi, nimestaafu nikiwa Brigedia Jenerali Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ). Sijui kama kuna mwanajeshi anayeogopa na hakuna mgombea
ninayemuogopa; nikiogopa ina maana mimi si mwanajeshi,” alisema na
kuongeza:
“Nina uzoefu wa kutosha, nina uwezo wa kuwatumikia Watanzania twende huko tunakotaka na kuinua uchumi wetu.
Nimejipima na nimeona nina uwezo wa kugombea urais kwa sababu
nakidhi vigezo vyote vinavyotakiwa kisiasa na kiuongozi; kilichonisukuma
kutangaza nia ya kugombea ni uwezo wangu, sijashinikizwa na mtu
yeyote,” alisema Jaji Ramadhani.
KUJIUNGA NA CCM
Kuhusu utata alijiunga lini na CCCM, wakati amekuwa mtumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 33, Jaji Ramadhani alisema:
“Nilijiunga na CCM mwaka 1969 nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu
Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na niliendelea na
uanachama wangu hadi 1992 kipindi mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa na
kusababisha mabadiliko ya Katiba ambayo yaliweka masharti kwa mtumishi
wa umma kutokuwa mwanachama.”
Jaji Ramadhani alisema baada ya mabadiliko hayo, uanachama wake
ndani ya CCM ulisimama hadi mwaka 2010 alipostaafu nafasi ya Jaji Mkuu
wa Tanzania na kulazimika kurejesha uanachama wake mwaka 2011 kwa ajili
ya kuendelea na masuala ya siasa.
“Nilirudia uanachama wangu wa CCM mwaka 2011, baada ya kustaafu wadhifa niliokuwa nao kama Jaji Mkuu”.
RUSHWA
Kuhusu rushwa, alisema ni tatizo kubwa nchini. “Tatizo la rushwa
katika serikali na nchi yetu ni kubwa, nataka nilimalize kama chama
changu kitaniteua na kushinda nafasi hiyo…wakati nilipokuwa Jaji Mkuu,
nilipambana nalo katika mahakama zetu,” alisema na kuongeza:
"Nawahakikishia Watanzania nikiwa Rais, ukila rushwa Kilimanjaro,
hutahamishiwa Mtwara maana hata waliopo Mtwara ni Watanzania, hawataki
mla rushwa.”
KATIBA MPYA
Alipoulizwa msimamo wake kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba
mpya, Jaji Ramadhani alisema: “Kwa nafasi yangu niliyokuwa nayo kama
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kazi yetu
ilikwishamalizika, baada ya kumkabidhi Rais Jakaya Kikwete, Rasimu ya
Pili ya Katiba pale kwenye ukumbi wa Karimjee na Bunge Maalum la Katiba
limemaliza kazi yake, hatua iliyobaki ni wananchi kuamua katika Kura ya
Maoni. Na ndiyo itakayoamua hatma ya Katiba Mpya na si Rais.”
|
June 18, 2015
JAJI MKUU MSTAAFU AJITOSA URAIS CCM.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment