![]() |
| Dk. Muzzammili Kalokola Kada wa CCM aliyetangaza nia ya kugombea urais kupitia chama hicho wiki iliyopita, Dk. Muzzammili Kalokola, juzi alijionja joto ya jiwe baada ya kupata kipigo kutoka kwa vijana wa ulinzi wa Green Guard wakati akisaka wadhamini mkoani Tanga.
Akisimulia mkasa huo kwa mwandishi wa NIPASHE kwa njia ya simu
jana, alisema , Jumatano baada ya kuwasili nje za ofisi hizo kama
alivyotakiwa na Katibu wa wilaya hiyo, ghafla alivamiwa na kundi la
Green Guard wakimtaka aondoke.
Alisema walimshambulia kwa kumpiga kisha kumkata mtama na
kudondoka, huku Katibu Mwenezi wa Wilaya, akitamka aondolewe katika eneo
hilo kwa madai kuwa ‘Mkutano hauwezi kuandaliwa na mwingine halafu mtu
mwingine azungumze’.
Tukio la shambulio hilo pia limeonyeshwa katika mitandao mbali
mbali ya kijamii, ambapo mtangaza nia huyo alionekana akipigwa na kundi
hilo na kuondolewa.
Alisema katibu huyo aliwaeleza vijana hao wamwondoe lakini akiwa
eneo hilo la tukio alimpigia simu katibu wa wilaya aliyemtaka awali
afike hapo saa 6:00 mchana kuomba udhamini.
“Wakati Katibu wilaya akija eneo la tukio, niliwasiliana pia na
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga (RPC) ambaye awali nilipeleka malalamiko
yangu kwake dhidi ya hujuma ninazofanyiwa,” alisema.
Alisema baada ya katibu wa wilaya kufika alimpa simu na kuzungumza
na RPC na baadaye alilazimika kwenda polisi na kupewa RB/Tan/58000/2015.
“Kada mwenzangu ndiye anayenichafua, maana nimefika hapa
nikavamiwa ghafla halafu jioni saa 12:00 huyo kada alikuja kuomba ridhaa
ya wadhamini,” alisema.
Akielezea hujuma alizofanyiwa, Dk. Kalokola alisema baada ya
kuchukua fomu Dodoma alipewa barua za utambulisho kwa kila katibu wa
mkoa ili wakasaini daftari la wageni na hatua nyingine zifuate.
Alisema mwanzoni mwa wiki hii alienda ofisi ya katibu wa wilaya
Tanga, ambapo huko alimkuta kaimu wake ambaye alimweleza kuwa, ofisi
inamtayarishia mtangaza nia Bernald Membe na Amina Salum Ali.
Alisema baada ya maelezo hayo, kesho yake alimwandikia barua Katibu
Mkuu wa chama Dodoma kwa sababu barua alizopewa zinaeleza wazi kuwa,
kila mtangaza nia atendewe haki.
Alisema siku hiyo wakati akijiandaa kwenda kwa RPC wa Tanga, ofisi ya wilaya iliwatuma watu wakamwite.
“Niliwajulisha kuwa nitaenda baadaye kwa sababu nilikuwa naenda
polisi, baadaye nilipoenda katibu wa wilaya sikumkuta nilirudi kesho
yake asubuhi nikaambiwa kesho yake niende kwa ajili ya kukutana na
wadhamini,” alisema na kuongeza:
“Kwa kuwa Alhamisi nilitakiwa kwenda Dar es Salaam kwenye kesi ya
katiba, nilimuomba ifanyike siku hiyo ya Jumatano, alikubali na kunitaka
saa 6:00 mchana nirudi ofisi hapo,” alisema.
Alisema muda ulipofika alienda ndipo alipoambulia kipigo hicho.CHANZO:NIPASHE
|
June 20, 2015
MTANGAZA NIA URAIS ASHAMBULIWA AKISAKA WADHAMINI.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment