![]() |
SERIKALI
imeahidi kukaa pamoja na vyama vya soka vya Tanzania (TFF) na Zanzibar
(ZFA) ili kuona uwezekano wa kuwa na chama kimoja kitakachoendesha
mchezo huo sehemu zote za Muungano.
Ahadi
hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Juma Nkamia wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa
Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM) aliyehoji uwezekano wa kuunganisha
vyama hivyo vya mpira kama ilivyo kwa Kamati ya Olimpiki (TOC) ambayo
sasa inaongozwa na Mzanzibari.
“Kuwa na
chama kimoja kama ilivyo TOC ni lazima tushirikishe wadau wote, tukae
pamoja na kuongea ili kusitokee malumbano. Ni wazo zuri, tumelipokea na
tutalifanyia kazi,” alisema Nkamia.
Kadhalika,
Nkamia alisema TFF muda wote imekuwa ikiunga mkono juhudi zozote
zinazofanywa na ZFA za kuwa mwanachama mshiriki wa Shirikisho la Soka
Duniani (FIFA) kama zilivyo ‘nchi’ zisizo na mamlaka kamili za Hong Kong
na Macau.
TFF pia imekuwa ikiunga mkono juhudi za ZFA kuwa mwanachama mshiriki wa Shirikisho la Soka la Afrika.
Nkamia
aliyasema hayo akijibu swali lingine la nyongeza la Mbunge wa Kilwa
Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM) aliyetaka kujua endapo kuna namna
yoyote ambayo TFF inaweza kuisaidia ZFA kuwa mwanachama wa Fifa.
Mapema,
Mbunge wa Kikwajuni, Hamad Yussuf Masauni (CCM), aliuliza kama
inawezekana kuwa na mashirikisho matatu nchini, yaani mbali na ZFA na
TFF kuwe na lingine litakalofanya kazi sehemu zote za muungano “ili
Wazanzibari nao wanufaike na misaada inayotolewa na Fifa.
Akijibu, Nkamia alisema hilo linaweza kuwa gumu kutokana na muundo wa muungano wa nchi yetu wa serikali mbili.
Katika
swali la msingi, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Jako Hashim Ayoub
alitaka kujua kwa nini uongozi wa sasa wa TFF ulikwenda Zanzibar na
kuidanganya ZFA kwamba utaipigania ipate uanachama Fifa wakati ukijua
haiwezekani kwa kuwa Fifa ilishasema Zanzibar haiwezi kupata uanachama
katika mfumo wa Muungano.
Akijibu
swali hilo, Nkamia alisema wizara yake haina taarifa juu ya ahadi
iliyotolewa na TFF kwamba ‘itahakikisha’ Zanzibar inapata uanachama
Fifa, bali kinachosisitizwa na TFF ni kuunga mkono juhudi zozote endapo
kutatokea mabadiliko katika taratibu za Fifa na hivyo kufungua milango
kwa ZFA kupata uanachama. (HABARI LEO)
|
June 17, 2015
SERIKALI KUFANYIA KAZI WAZO LA ‘TFF’ MOJA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment