Basi la Fahisan Huwei, likiwa limeharibika baada ya kugonga treni ya
abiria katika kijiji cha Kibaoni wilayani Kilosa jana. PICHA: Ashton
Balaigwa Watu
wanne, akiwamo baba na mtoto wake mwenye umri wa miaka sita, wamekufa
papo hapo na wengine 33 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Fahisan
Huwel, walilokuwa wakisafiria kugonga treni la abiria mali ya Kampuni
ya Reli Tanzania (TRL) katika Kijiji cha Kibaoni wilayani hapa, Mkoa wa
Morogoro.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa mkoa huo, Musa
Malambo, ajali hiyo ilitokea jana saa 1.30 asubuhi, wakati basi hilo
aina ya Isuzu Jouney likitokea Kijiji cha Tindiga wilayani humo kwenda
mjini Morogoro.
Malambo alisema basi hilo lilipofika katika eneo hilo, liligonga
treni hilo lililokuwa likitokea jijini Dar es Salaam kwenda Mkoa wa
Kigoma kisha kupinduka mara mbili na kusababisha vifo hivyo na majeruhi
hao.
Alitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa dereva wa basi hilo
lenye namba T837 CTN, Bakari Salehe Nyange, Mkazi wa Kilosa, kushindwa
kuchukua hadhari alipofika kwenye eneo la makutano ya reli na barabara.
Aliwataja waliokufa kuwa ni Sarehe Gomba (35), Mkazi wa kijiji cha
Tindiga; Mama Husna (33), wa Mamoyo; mtoto huyo Surati Mwajili (6) na
baba yake aliyefahamika kwa jina moja na Mwajili (38), wakazi wa Pugu
jijini Dar es Salaam .
Alisema wanamshikilia dereva wa basi hilo ambaye ni mmoja wa
majeruhi wa ajali hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, ambako
amelazwa kwa matibabu.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya hiyo, Dk. Dennis Ngaromba,
amethibitisha kupokea maiti wanne na majeruhi hao, akisema baadhi ya
wametibiwa na kuruhusiwa kutokana hospitalini kutokana na hali zao kuwa
nzuri.
Alisema majeruhi watano hali zao mbaya kutokana na kujeruhiwa
vibaya kifuani na kichwani huku wengine wakiwa hawana fahamu na
kuwahamishia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu
zaidi.
Mmoja wa abiria wa basi hilo, Rajabu Abdallah, alisema tangu
walipoanza safari katika kijiji cha Tindiga, dereva wa basi hilo
alibadili njia ya kawaida ya Kibaoni, Mamoyo, Mabwegere na kupitia
Kimamba na kwamba kutokana na mvua kunyesha, aliamua kutumia njia fupi
ya Kipolelo yenye makutano na reli.
Alisema akiwa katika njia hiyo alikuwa kiendesha basi hilo kwa
mwendo kasi bila ya kuchukua tahadhari ya alama kwenye makutano ya reli
na barabara na kuligonha treni hilo.
Alisema baada ya kutokea ajali hiyo, dereva wa treni hilo lenye
namba 8U03 , Ainea Chipindula, Mkazi wa Morogoro, alisimama na kuwabeba
majeruhi hadi Kilosa mjini kisha kukimbizwa hospitali ya wilaya hiyo
kwa matibabu.
CHANZO:
NIPASHE
|
July 2, 2015
BASI LAGONGA TRENI, WANNE WAFA, KUJERUHI 33.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment