Mbatia |
Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) umethibitisha tetesi zilizokuwa zikijadiliwa kwenye mitandao ya
kijamii nchini juu ya Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kujiunga na
umoja huo ili kugombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
25 mwaka huu.
Tamko lililosainiwa na
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia kwa niaba ya wenyeviti wenza wa
umoja huo wameamua kumkaribisha Lowassa ili aungane nao kwakuwa ni
mchapa kazi
Amesema Watanzania wanataka
mabadiliko yatakayoibua demokrasia ya kweli kuachana na uonevu,
udhalilishaji, na majungu unaoendelezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Tunaamini Lowassa ana uwezo wa
kuhamasisha umma kuikataa CCM yenye kusimamia mifumo isiyotenda haki,
mfuatiliaji wa karibu wa utendaji katika majukumu anayokabidhiwa,”
Mbatia ameongeza katika ofisi za Chama cha Wananchi (CUF) akiwa na
wenyeviti wenza Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF)
na Emmanuel makaidi (NLD).
“Katika kutafakari kwa kina
maslahi ya taifa letu, Ukawa tunahitaji viongozi wenye sifa, uwezo na
weledi katika kulinda, kuheshimu na kusimamia rasilimali za taifa kwa
maslahi ya Watanzania wote,” alisema Mbatia.
Baada ya kutoa tamko hilo mbele
ya waandishi wa habari Mbatia aliulizwa ikiwa wanakumbuka namna
viongozi wa vyama vya upinzani walivyomnyooshea kidole Lowassa kutokana
na kashfa ya ufisadi Richmond iliyomfanya kujiuzulu wadhifa wake mwaka
2008.
Mbali ya Richmond, Katibu Mkuu
wa Chadema Dk. Wilbroad Slaa akiwa katika uwanja wa Mwembeyanga Temeke
jijini Dar es Salaam alitaja orodha ya majina 11 ya mafisadi jina la
Lowassa likiwemo je ikiwa kiongozi huyo atajiunga na Ukawa watawaambia
nini Watanzania kuhusiana na usafi wake.
Mbatia alisema, “Ufisadi ni masuala ya kimfumo, mfumo uliopo CCM ndio unaolea ufisadi.
Emmanuel Makaidi alisema Ukawa hawawezi kuthibitisha kama Lowassa ni fisadi au la mpaka vyombo vya sheria vitakapomtangaza.
“Kuna watu wengi wapo gerezani
na wengine kesi zinaendelea mahakamani kutokana na ufisadi, lakini
hatujaona kesi ya Lowassa utasemaje ni fisadi,” alisema Makaidi.
Kuhusu nafasi ya Lowassa
kugombea urais kupitia Ukawa Profesa Lipumba alisema kwa sasa
hawajampitisha moja kwa moja, lakini atakapokubali kujiunga watakaa na
kujadiliana kwa mujibu wa katiba yao halafu watajua kama awe mgombea wao
au vinginevyo.
No comments:
Post a Comment