KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

July 7, 2015

ZENGWE DHIDI YA LOWASSA LASUKWA

Lowassa
Wakati joto la uchujaji wa majina ya wagombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) likizidi kuongezeka, taarifa zimezidi kuzagaa mitaani na kwenye mitandao ya kijamii kwamba, mikakati ya kumuondoa Edward Lowassa kwenye orodha ya watia nia nayo imezidi kupamba moto.
 
Kwa muda sasa NIPASHE imekutana na makundi mbalimbali ya wasaka urais na ajenda kuu inayozungumzwa ni mizengwe ya kumwengua Lowassa kwenye kinyang’anyiro hicho ili kuwarahisishia wengine njia ya kuteuliwa na chama kwa kuwa anaonekana kuwa kikwazo kwa baadhi ya washindani wake.
 
Ofisa mmoja wa CCM makao makuu mjini hapa, aliiambia NIPASHE kuwa wanachofanya wao kama watendaji ni kuandaa majina ya wagombea wote na fomu zao za udhamini na kisha kukabidhi kwa sekretarieti itakayopanga ajenda za vikao vya Kamati Kuu na baadaye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya taifa.
 
Ofisa huyo alipoulizwa kama ana taarifa za kuwako kwa mizengwe dhidi ya Lowassa alisema kwa ujumla kwa sasa kuna maneno mengi sana yanazungumzwa juu ya mchakato wa uteuzi wa mgombea, ila akasisitiza kuwa la msingi ni kusubiri vikao vya maamuzi.
 
“Ndugu yangu ukiyatazama haya makundi (ya urais) ni vigumu kuamini kama wanatoka chama kimoja. Yaani kuna kukamiana kweli kweli. 
 
Kila mmoja anataka kumwangusha mwenzake ili yeye apite,” alisema na kuongeza kuwa:
“Hata kama kuna mizengwe, si unajua uchaguzi huu ni wa vyama vingi. CCM haishindani pekee yake, kwa hiyo mgombea anayekubalika ndiye anatakiwa.”
 
Hata hivyo, kwa muda sasa kumekuwa na mfululizo wa habari za kupikwa kwamba jina la Lowassa litaishia Kamati Kuu kwa madai kwamba kuna ushahidi wa matumizi ya fedha kwa timu yake, tuhuma ambazo binafsi (Lowassa) amezikanusha mara kadhaa. Julai mosi mwaka huu siku anarejesha fomu za kuwania urais kupitia CCM alitoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa kuhusika kwake na rushwa ajitokeza na kusema alitoa lini, wapi na kwa nani.
 
Akizungumza na mamia ya wanachama wa CCM makao makuu Dodoma siku hiyo, mbali ya kuwashukuru wote waliomdhamini, Lowassa alisema amechoka kwa tuhuma za kipuuzi za kuhusishwa na rushwa na kusisitiza kuwa hakuna mwanachama yeyote miongoni mwa zaidi ya nane waliomdhamini aliyefanya hivyo kwa kishawishi cha fedha au fadhila yoyote.
 
NIPASHE imedokezwa kwamba miongoni mwa mikakati inayosukwa kumwangamiza Lowassa ni pamoja na kutengenezwa kwa taarifa za mawasiliano ya siku kuonyesha kwamba kuna fedha nyingi zimetumwa kwa wanachama wa CCM ili kuwashawishi kumuunga mkono.
 
Mgombea anayetajwa kutumiwa zaidi na kundi linalompinga Lowassa ni pamoja na Makongoro Nyerere, ambaye alifanya mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni na kuporomosha kauli kali za ukakasi dhidi ya Lowassa.
 
Wakati mizengwe ikizidi kusukwa dhidi ya Lowassa, ripoti ya kura zote za maoni ambazo zimekuwa zikitolewa katika miezi ya hivi karibuni zimeonyesha kuwa Lowassa anaongoza kwa mbali kama chaguo la wananchi wengi kwenye nafasi hiyo.
 
Miongoni mwa tafiti hizo ni ule wa Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uliofanywa mwezi uliopita na matokeo yake kutolewa mwishoni mwa wiki unaonyesha kuwa Lowassa ni changuo la kwanza la wengi kwa kujipatia asilimia 27.0 ndani ya chama hicho, huku Bernard Membe akishikilia nafasi ya pili kwa kupata asilimia 8.2.
 
Katika utafiti huo ambao REDET walisema kuwa unaweza kuchukuliwa kwa ujumla wake kama maoni ya Watanzania endapo masuala yaliyoulizwa uchaguzi ungefanyika katika kipindi cha utafiti, wahojiwa walikuwa 1,250 kutoka wilaya moja moja katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.
 
Wakati mkakati wa mizengwe ukiendelea kupamba moto, wajumbe wa sekretarieti ya Kamati Kuu ya chama hicho wanaanza vikao mjini hapa leo kundaa pamoja na mambo mengine ajenda na taarifa kwenye vikao vya Kamati Kuu itakayokaa Alhamisi mjini hapa.
 
Kikao cha Kamati Kuu kinatarajiwa kuchuka majina ya watia nia 38 waliojitokeza kutafuta ridhaa ya chama hicho na kubakisha majina matano tu yatakayopelekwa NEC kwa kupigiwa kura.
 
NEC inayotarajiwa kukutana Ijumaa wiki hii, itatoa majina matatu kwenda Mkutano Mkuu unaotarajiwa kukutana Jumamosi kwa ajili ya kupata jina moja la mgombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment