PUBLIC NOTICE BASATA LATAKA KUONDOLEWA/KUSITISHWA MARA MOJA KUCHEZWA KWA NYIMBO ZOTE ZENYE KUKENGEUKA MAADILI, SHERIA NA TARATIBU
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) linawaagiza wasanii, wamiliki na waendeshaji
wa wavuti, tovuti na vyombo vya habari hususan radio na runinga kuondoa
na kuacha mara moja kurusha au kutangaza au kucheza nyimbo zote zenye
maudhui ya kashfa, matusi, kejeli, udhalilishaji ambazo zinahatarisha
kuigawa jamii ya kitanzania katika misingi yoyote hasa katika kipindi
hiki Taifa linapoendelea na kampeni za kisiasa na kujiandaa na uchaguzi
mkuu.
Kwa mujibu wa kifungu namba 118 (a-d) cha Sheria ya
Bunge namba 9 ya Mawasiliano ya Mtandao ya mwaka 2010 ni marufuku kwa
njia yoyote kwa mtu au chombo chochote kutengeneza, kuzalisha, kusambaza
au kutangaza ujumbe ambao una mlengo wa matusi, dharau, uzushi au jinai
kwa lengo la kutukana, kutisha, kusumbua au kushusha hadhi ya mtu
mwingine.
Aidha, Sheria ya Bunge namba 4 ya Makosa ya Mtandao
ya mwaka 2015 kifungu cha 45 (1) (a-c) kinatoa mamlaka kwa taasisi au
mtu yeyote anayebaini uvunjifu wa Sheria katika mitandao kutoa notisi
kwa yeyote yule anayesambaza au kutangaza ujumbe au maudhui yanayovunja
sheria za nchi kuacha mara moja au vinginevyo hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya yeyote anayekaidi.
Ni kwa msingi huu,
BASATA linawaagiza wasanii, wamiliki wa wavuti, tovuti na wale wenye
akaunti kwenye mitandao ya kijamii kama sound cloud, U-Tube, ITunes nk.
kuondoa ndani ya siku saba (7) kuanzia siku ya kwanza ya taarifa hii
nyimbo zote zinazokengeuka maadili na kubeba mlengo wa matusi, kashfa,
kejeli na udhalilishaji wa watu wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa
kisiasa na kitaifa.Aidha, BASATA linawakumbusha tena Wasanii wote
nchini kuacha mara moja kubuni na kutengeneza kazi za Sanaa zenye
kuashiria kuigawa jamii katika misingi yoyote ya kibaguzi na zaidi
kutumia Sanaa kubomoa jamii badala ya kuijenga.
BASATA
linawasisitiza wamiliki wa vyombo vya habari hususan radio na runinga
pia watangazaji na Ma DJs kuhakikisha hawawi chanzo cha kusambaza
maudhui yoyote ya Sanaa yenye mlengo wa kuibua chuki, matusi, kashfa na
mgawanyiko wa Taifa.
BASATA kwa mamlaka yake chini ya Sheria
namba 23 ya mwaka 1984 na yale ya Sheria ya Mawasiliano ya Posta na
Mitandao ya mwaka 2010 na ile ya Makosa ya mitandao ya mwaka 2015 kwa
kushirikiana na vyombo vya dola halitasita kuchukua hatua kali za
kisheria na kinidhamu kwa wasanii, wamiliki wa wavuti, tovuti na vyombo
vya habari ambavyo vitaendelea kutangaza na kusambaza nyimbo zenye
mwelekeo wa kuhatarisha usalama, umoja na mshikamano wa Taifa.
BASATA
likiwa ni msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linatambua
kwamba Sanaa ikitumiwa kwa ukengeufu inaweza kuwa chanzo kikuu cha
machafuko, mivurugano na kupotea kwa amani nchini. Hivyo umakini
unahitajika miongoni mwa wasanii katika kuzingatia weledi, maadili,
uzalendo kwa taifa na kuitumia Sanaa kama chombo cha kujenga jamii yenye
kuzingatia maadili.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI.



No comments:
Post a Comment