![]() |
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema, Edward Lowassa akihutubia umati wa wananchi katika kampeni zake zinazoendelea. |
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), anayeungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa,
Edward Lowassa amewaahidi wakazi wa Mtwara kuwa endapo atachaguliwa kuwa
rais, ataunda tume maalumu kuchunguza mikataba ya gesi asilia.
Lowassa alisema kuwa kwa kuwa gesi sasa imeshatoka kwenda Dar es
Salaam, si wakati tena wa kupinga isitoke, lakini ipo haja kwa serikali
yake atakayoiunda, kuchunguza mikataba yote ya gesi ili kujiridhisha
kama haikuingia kwa hila. “Ndugu zangu wa Mtwara gesi inatoka,
haitokiiiiii?....inatokaaaaaaa?.
Ngoja niwaambieni hivi, mkinichagua kuwa rais nitaunda tume maalumu
ambayo itachunguza mikataba yote ya gesi ili kujiridhisha kama ilikuwa
sahihi au hapana ;na watakaohusika tutawafikisha katika vyombo vya
sheria, washughulikiwe kwa mujibu wa sheria,” alisema Lowassa.
Lowassa aliyasema hayo baada ya mamia ya watu wakazi wa Mtwara,
waliofika katika mkutano wake kumsikiliza kumhoji kwa nini hazungumzii
suala la gesi. Walifanya hivyo baada ya Lowassa kuonekana kumaliza
hotuba yake, bila kulitaja suala hilo, ambalo wakazi wa Mtwara wanadai
ni ajenda yao.
“Nadhani tumeelewana, eti upande ule kule mmenielewa suala hili la
gesi? Nataka tulimalize kwa namna hii, sawaa?...lazima tuwashughulikie
waliohusika kama vyombo vitawaona wana hatia”, alisema Lowassa.
Awali, mgombea huyo aliwaahidi wakazi wa Mtwara kuwa serikali
atakayoiunda, itakuwa makini na itahakikisha hakuna hata mtanzania
mmoja, atakayekuwa masikini katika kipindi kifupi cha uongozi wake.
“Nachukia umasikini, ndio maana nimegombea nafasi hii...nataka kwa
aliye na baiskeli moja, anunue ya pili ;na kama unakula mlo mmoja ule
milo mitatu ;na aliye na mke mmoja aoe wa pili kama dini yake
inamruhusu,” alisema Lowassa.
Alisema atatengeneza mazingira mazuri kwa mamantilie, bodaboda na
wamachinga ili wafanye kazi zao kwa tija. Akimkaribisha Lowassa
kuzungumza na wananchi, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye alisema
kuwa CCM imeshindwa kuwaletea maendeleo wananchi kwa haraka; na inapaswa
kuondoka madarakani kumpisha Lowassa, alete maendeleo kwa haraka.
Kabla
ya kufanya mkutano wake mjini Mtwara katika viwanja vya Mashujaa,
Lowassa alihutubia mikutano miwili katika wilaya za Newala na
Tandahimba.
No comments:
Post a Comment