![]() |
Waziri Mkuu Mstaafu wa awamu ya tatu, Fedrick Sumaye amesema
kama Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utakuwa huru na haki, basi umoja wa vyama
vinavyounda Ukawa watashinda na kuingia madarakani.
Sumaye amesema ana uhakika
kwa asilimia kubwa upinzani wana nafasi kubwa ya kushinda Katika uchaguzi mkuu
ujao ni ndio sababu mojawapo iliyomfanya ajitoe CCM na kujiunga upinzani.
Akihojiwa katika kipindi cha Funguka kilichorushwa na kituo cha televisheni cha
Azam Tv, Sumaye ambaye alikuwa waziri mkuu kwa miaka kumi katika serikali ya
awamu ya tatu amesema amejitoa CCM kwa sababu ameona hali ndani ya chama hicho
si nzuri na kuwa kuna nafasi kubwa ya upinzani kuingia madrakani.
Sumaye
alisema hajajiunga na upinzani kwa kuahidiwa madaraka yoyote na kwamba lengo
kubwa ni kutoa ushauri kwani anaamini ana uzoefu mkubwa wa kuitawala na atakuwa
msaada kwao.
Akizungumzia kuhusu ufisadi ambapo awali alikaririwa akisema
atatoka CCM endapo chama hicho kitamchagua fisadi, Sumaye alisema hana tatizo
na Dk Magufuli lakini mfumo mzima wa chama na kuongeza kuwa hajawahi mahali
popote kumtaja kwa jina Lowassa kuwa ni fisadi.
“Vita yangu ya ufisadi nimeanza
maisha yangu yote na hakuna mahali popote nimewahi kumtaja Lowassa kuwa ni
fisadi, taarifa ya Bunge haijawahi mtaja Lowassa kushiriki jinai yoyote katika
suala la Richmond,” alisema Sumaye.
Kuhusu umiliki wa ardhi kubwa huku wananchi
wengi wakilia hawana ardhi, Sumaye alisema haoni tatizo lolote kumiliki ardhi
kihalali huku akisema eneo la hekari 300 analomiliki ni kidogo ikilinganishwa
na vigogo wengine.
“Kama ukitupanga viongozi na kuangalia ukubwa wa mashamba
tuliyonayo, mimi nitakuwa mkiani,” alisema Sumaye na kuongeza: “Hivi kuwa na
shamba ni dhambi? Nchi yeyote inayoendelea, watu ambao watabaki kwenye kilimo
watakuwa na ardhi kubwa.” Sumaye aliongeza kusema kuwa hata kama Ukawa
hawataingia madarakani, hatarudi tena CCM na ataendeleza upinzani.



No comments:
Post a Comment