![]() |
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amesema
taifa linakabiliwa na viashiria vya uvunjifu wa amani kutokana na kuwapo kwa
mgawanyiko wa kijamii unaosababishwa na watu kupandikiza mbegu za chuki na
kukithiri maneno ya uongo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi kwenye
uzinduzi wa Chama cha Wajasiriamali Wanawake (Vowet), Dk. Mengi alisema tatizo
hilo ni sawa na saratani inayopaswa kuogopwa na kuomba kila Mtanzania kwa imani
yake kuomba kwa Mungu ili upendo uzidi kuimarika na amani idumu nchini.
Katika
hafla hiyo, Dk. Mengi pia alizindua Chama cha Wajasiriamali Wanawake (Vowet) na
kukabidhiwa tuzo ya kumtambua kama mpigania amani na mjasiriamali mwenye
mafanikio. Alisema kuongezeka kwa vitendo vya chuki ndani ya jimii, ni ushahidi
kwamba upendo na mshikamano uliodumu kwa miaka mingi unaanza kutoweka nchini.
“Nawaomba Watanzania kurudisha upendo, kila mmoja kulingana na imani yake
tumuombe Mungu, kama wewe ni Muislamu au Mkristo rudini katika vitabu
vitakatifu ili kuhamasisha amani na upendo,” alisisitiza Dk. Mengi na kuongeza:
“Wananchi wamevunjika moyo baada ya kuona viongozi wenye dhamana wanakuwa
sehemu ya matatizo kwa kuhusishwa katika vitendo vya rushwa na ufisadi.
”
Alitaka viongozi kuheshimu na kufuata utawala bora kwa kuzingatia uwazi,
kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyatatua. “Viongozi wawe wepesi kutatua
matatizo ya wananchi, kusubiri mpaka maandamano na migomo ni kitu kisichotakiwa
kwa sababu vitendo hivyo ni uvunjifu wa amani na vinaweza kusababisha vurugu
kubwa nchini,” alisema.
“Amani ikitoweka sote tutaumia lakini wanawake, watu
wenye ulemavu, watoto na wagonjwa ndio watakaoathirika zaidi, pia itaathiri
shughuli zote za uchumi, biashara na shughuli za kiserikali.” Aidha, Dk. Mengi
aliwataka wanawake kujikita katika ujasiriamali, akisema utawapa uwezo wa
kujitegemea pamoja na kupunguza unyanyasaji wa kijinsia dhidi yao, kujenga
mazingira ya heshima na usawa kati yao na wanaume.
Aliwatia moyo wanawake kwa
kuwataka kutokata tamaa na badala yake siku zote wajiamini kwamba wanaweza na
watafika mbali kimaendeleo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Vowet,
Maida Waziri, alisema mkutano huo uliandaliwa kwa ajili ya kuwatia moyo
wanawake wajasiriamali pamoja na kuwakumbusha wajibu wao katika kuitunza amani.
Alisema wanawake ndiyo msingi wa maendeleo ya Tanzania na hata katika kipindi
cha kupigania uhuru, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwatumia kama
sehemu muhimu ya uelimishaji jamii.
“Hatutaki kuwa sehemu ya watu watakaovunja
amani kwa sababu tunatambua sisi (wanawake) ndiyo waathirika, tunahitaji
uchaguzi mkuu upite ukituacha tukiwa watulivu, wamoja na amani itamalaki,”
aliongeza kusema Maida.



No comments:
Post a Comment