Wilbert Molandi na Gladness Mallya
NAHODHA na beki wa kati wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa,
siku kadhaa zilizopita alivamiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi na
kujaribu kuiba fedha.
Beki huyo, aliyevamiwa nyumbani kwake Mapambano, Sinza jijini
Dar es Salaam, anakumbukwa kwa kuweka rekodi ya kuwatoa Zamalek katika
michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003.
Simba iliwatoa Zamalek kwa njia ya penalti baada ya mechi ya nyumbani
kuwafunga bao 1-0 kabla ya kwenda kurudiana Cairo, Miri na kufungwa bao
1-0 kabla ya kwenda hatua ya penalti na kuwatoa baada ya Juma Kaseja
kupangua penalti kisha marehemu Christopher Alex kufunga tuta la
ushindi.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Pawasa alisema majambazi hao watatu
walimvamia saa 11:30 alfajiri nyumbani kwake na kumtaka atoe fedha
alizonazo.
Pawasa alisema, majambazi hao inavyoonekana kama walipewa taarifa za
yeye kuwa na fedha nyingi alizopewa akaweke benki na mmoja wa
wafanyabiashara wenzake aliyemtaja kwa jina moja (linahifadhiwa) siku
moja kabla ya tukio hilo.
“Inavyoonekana kama dili vile limechongwa na watu flani waliokuwa
wanajua nina fedha nyingi nilizotoka nazo ofisini na kurudi nazo
nyumbani kwa ajili ya kuzihifadhi.
“Kwa sababu hao majambazi walipovamia tu nyumbani kitu cha kwanza
kuniambia ni tumefuata fedha zetu, kwa maana ya zile nilizopewa na jamaa
yangu ninayefanya naye biashara, kitu ambacho ni cha kweli lakini
tayari nilikuwa nimeshazipeleka fedha hizo benki.
“Majambazi hao walikuwa watatu, kati ya hao wawili nilikuwa napambana nao mlangoni wakitaka kuingia ndani.
“Wakati napambana na majambazi hao wawili, mmoja alitoa bunduki na
kunipiga na kitako chake na kunipasua usoni, bila kujali nilijaribu
kupambana nao hivyohivyo kuhakikisha ninaokoa uhai wangu.
“Baada ya kuona nimewashinda walitoka nje na kukimbilia bodaboda
waliyokuja nayo iliyokuwa imeegeshwa nje, mmoja alidondoka, nikafanikiwa
kumkamata, muda huo tayari majirani walikuwa wameshasogea baada ya
kusikia makelele.
“Tulivyomkamata majirani walimshambulia na baadaye kumpeleka kituo
cha polisi kabla ya kupelekwa mahabusu Gereza la Segerea huku wenzake
wakitafutwa.
“Baada ya purukushani hizo kumalizika nilienda Hospitali ya Palestina,
Sinza kwa ajili ya matibabu, nimeshonwa nyuzi tatu ambazo nimetolewa
juzi,” alisema Pawasa.KWA HISANI YA GLOBAL PUBLISHERS
|
No comments:
Post a Comment