Gavana wa Jimbo la Siaya, nchini Kenya, Cornel Rasanga ameingia
matatani akidaiwa kutumia Sh20 milioni za nchi hiyo (karibu Sh400
milioni) kutoka katika mfuko za Serikali kwa ajili safari ya kuhudhuria
sherehe za kumwapisha Rais John Magufuli.
Dk Magufuli alipishwa
Novemba 5, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam baada ya Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika
Oktoba 25.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali Kenya (PAC), Nicholas Gumbo amemtuhumu
Rasanga kwa kutumia fedha hizo kutoka kwenye mfuko wa Serikali wa
safari.
“Gavana wa Rasanga
lazima awaambie wananchi wa Siaya, imekuwaje akatumia Sh20 milioni
kwenda Tanzania kwa ajili ya shughuli ya Dk Magufuli?
“Sidhani kama Dk
Magufuli ana uhusiano wowote na wananchi wa Kaunti ya Siaya kiasi cha
Gavana kutumia fedha hizo za umma kwenda Tanzania,” alisema Gumbo.
Gumbo alisema Dk
Magufuli anafahamika kuwa ni rafiki mkubwa wa kiongozi wa Cord, Raila
Odinga ambaye pia alihudhuria sherehe hizo.
Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wa Afrika.
Akizungumzia tuhuma
hizo, Rasanga alisema madai yalitolewa na Gumbo ambaye ni Mbunge wa
Rarieda, ni uzushi na alikuwa anataka kujikweza kisiasa.
“Hii ilikuwa safari binafsi. Hatukutumia fedha za Serikali kama inavyoelezwa,” alisema alipohojiwa na gazeti la Daily Nation.
Gavana huyo alisema alikwenda kuhudhuria kuapishwa kwa Dk Magufuli kwa mwaliko binafsi wa Rais hiyo wa Tano wa Tanzania.
Hata hivyo, alisema ziara yake Tanzania itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza ushirikiano katika Ukanda wa Ziwa Victoria.
“Ukweli ni kwamba Rais
wa Tanzania aliwahi kutembelea Siaya na tulijadiliana masuala mbalimbali
ikiwamo usafiri hasa katika Ziwa Victoria,” alisema Rasanga na
kuongeza:
“Dk Magufuli anatokea
Kanda ya Ziwa na mpango wake mkubwa ni kuimarisha bandari katika Ziwa
Victoria na kuchaguliwa kwake kuwa Rais kutarahisisha zaidi utekelezaji
wa mipango yake.
“Hakuna sababu ya
kuingiza siasa katika safari hii. Tuko katika mipango mizuri tu ya
kibiashara na Tanzania ambayo kwa sasa imeanza kupanuka.”
Mwenyekiti huyo wa PAC Kenya alisema safari hiyo ya Novemba 5, ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Hata hivyo, Naibu Gavana, Wilson Ouma alipinga madai ya Gumbo akisema alikuwa na lengo la kumharibia bosi wake.
“Ukweli Gavana Rasanga
alitumia fedha zake kwenda Tanzania na uzushi wowote unatakiwa
ukomeshwe,” alisema Ouma alipozungumza na Nation.
Akisisitiza, Gumbo
alisema ataendelea kupambana na matumizi mabaya ya fedha za umma
unaofanywa na maofisa wa Serikali kwa kutumia vyeo vyao.
Magufuli kivutio nchi jirani
Madai hayo yameibuka
wakati kasi ya utendaji wa Rais Magufuli tangu aapishwe ikizidi kuwa
kivutio katika mitandao mbalimbali ya kijamii nchini Kenya na katika
nchi nyingine jirani.
Kwa kipindi cha takriban
siku 20 alizokaa ofisini, Rais Magufuli amechochea utendaji katika
utumishi wa umma na kupunguza gharama akianza kwa kukata safari za nje
kwa watumishi wa umma na sherehe za uhuru.
Kutokana na utendaji
huo, watumiaji wa mtandao wa Twitter walianza kutumia kwa kasi
kiunganishi cha “#Magufuli” huku kwa sehemu kubwa, raia wa Kenya
wakiongoza mjadala hadi jana jioni.
Raia hao walionekana
kuvutiwa na utendaji katika siku za awali za Dk Magufuli huku wakikosoa
Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta wakidai inazidi kukithiri kwa rushwa.
“Hello Tanzania, Kenya
inataka imkodi #Magufuli kwa wikiendi moja,” aliandika kwa Kiingereza
mtumiaji wa Twitter mwenye jina la Ezekiel Mogaka kutoka Kenya.
Lakini mtumiaji mwingine
mwenye akaunti yenye utambulisho wa Chakkah Dan aliandika; “Rais
Magufuli bila shaka (Hayati Baba wa Taifa), Julius Nyerere anatazama
chini kutoka peponi akiwa anajivunia utendaji wako.
“Watanzania wanaamka
kila siku asubuhi wakiona jambo fulani limetekelezwa na #Magufuli lakini
Wakenya wanakwenda kulala na jambo ambalo #Kenyatta kaahidi,” aliandika
The Golden Voice.
Kwa mujibu wa mtandao
unaofutilia mijadala kwenye Twitter nchini Kenya, #GURUS daily trend,
tangu jana asubuhi, kiunganishi “#Magufuli” kilikuwa ni miongoni mwa
viunganishi vitano vilivyokuwa vinaongoza kwa kuchangiwa, vingine ni
#WhatBalalaShouldDo, #YouDontKnowLifeStruggle, Welcome to Kenya, Turkey
na #FagiaKenya.
Katika mijadala hiyo,
Wakenya walikuwa wakijaribu kufananisha siku 19 za Rais Magufuli na
miaka mitatu ya Rais Kenyatta na kutania kuwa iwapo Rais wa Tanzania
angegombea mwaka 2017 nchini humo bila shaka wangemchagua.
Mijadala hiyo
‘haijabamba’ Kenya pekee, Burundi nao hawakuwa nyuma. Mwenye akaunti
yenye jina Joseph Siboma aliandika: “Wakati ukomo wa madaraka
ukiheshimika Tanzania, namkaribisha #Magufuli atawale kwa vipindi
visivyoisha #Burundi.”
Mhadhiri wa Sayansi ya
Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda, alisema nchi
nyingi za Afrika zinahitaji kuwa na viongozi wanaojali masilahi ya
wananchi lakini historia inaonyesha sehemu kubwa ya viongozi waliopo
madarakani ni watawala wasiojali watu wao na hawapendi kuharibiwa nafasi
zao.
“Sasa inapotokea kuna
kiongozi kama Rais Magufuli anayepunguza matumizi ya Serikali bila shaka
atakonga nyoyo za wengi. Mtindo wa uongozi wa Rais ni mpya na katika
mambo yote aliyoyafanya hakuna wanaopinga zaidi ya kuwapo wachache
wanaoonya mwenendo huo uendelee bila kupungua kasi,” alisema Mbunda.


No comments:
Post a Comment