Rais John Magufuli jana aliamua kuwatolea uvivu wadau waliopinga kitendo
chake cha kutumia hadhara kumsimamisha kazi mkurugenzi wa Jiji la Dar
es Salaam, Wilson Kabwe.
Rais alimsimamisha kazi Kabwe baada ya
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumchongea mtendaji huyo wa
jiji kuwa alisaini mikataba miwili ya huduma za usafiri na kusababisha
jiji lipoteze mabilioni ya fedha.
Baada ya kusikilia maelezo
hayo ya Makonda, Rais Magufuli aliuliza wananchi waliohudhuria hafla ya
uzinduzi wa Daraja la Mwalimu Nyerere kuwa achukue uamuzi gani na
kujibiwa ‘mtumbue’, na hapo hapo akatangaza kumsimamisha kazi kwa
uchunguzi.
Kitendo hicho kimepingwa na wadau mbalimbali wa haki
za binadamu na utawala bora, ambao walisema kuwa Rais
alitakiwa kwanza kupokea taarifa hiyo na kufanya uchunguzi ambao ungempa
Kabwe haki yake ya msingi ya kusikilizwa kabla ya kusimamishwa kwa
tamko la hadharani.
Jana, akiongea na viongozi wa ngazi tofauti
wa CCM katika hafla ya kuwashukuru kwa kazi waliyoonyesha wakati wa
Uchaguzi Mkuu uliopita, Rais Magufuli alisema kama watu anaowatumbua
hadharani pia waliiba hadharani, ni lazima watumbuliwe hadharani.
Magufuli
alisema kuwa mateso waliyopata
mamilioni ya Watanzania kutokana na kuibiwa, yanafanywa na hao wachache
lazima nao waanze kupata mateso hayohayo.
“Kwa hiyo ziko haki za binadamu kwa matajiri tu kwa hawa walioibiwa hakuna haki,” aliuliza Rais Magufuli.
“Kwa
hiyo unaweza kuona hawa wanaowatetea nao ni majipu. Tutaanza
kuwafuatilia. Hata ukimtoa huyo, nikimsema hadharani wanasema eti
nimefanya kosa.”
Rais Magufuli alisema kwa bahati nzuri
aliwateua yeye na kuwatangaza hadharani, hivyo akahoji sababu za
kutotangazwa hadharani siku ya kutenguliwa kwa kuwa ndiyo saizi yake
aliyewateua.
“Kama ni mkurugenzi wa manispaa au wa wapi
nimemteua mimi. Eti wanasema apewe muda wa kujieleza. Ajieleze yeye
aliwapa muda wananchi kujieleza alipokuwa anawaibia? Napenda
niwahakikishie tutaendelea kusimama imara,” alisema Dk Magufuli |
No comments:
Post a Comment