![]() |
Anitha Jonas – MAELEZO
TANGU enzi za Azimio la Arusha,
suala la maadili limekuwa likisisitizwa kama nguzo muhimu katika utoaji
wa huduma kwa umma. Lengo lilikuwa ni kuhakakisha kwamba kila mtumishi
wa Umma anatekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo
iliyowekwa.
Kutofanikiwa kwa Azimio la
Arusha kulitokana na baadhi ya Viongozi kujua kwamba utekelezaji wa
malengo ya azimio hilo ungekwamisha nia ovu waliyokuwanayo kama
Watumishi wa Umma katika kuwahudumia Wananchi. Ndio maana juhudi ya
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kutaka azimio
hilo liungwe mkono hazikuzaa matunda.
Pamoja na kuwepo sheria,
kanuni, miongozo na mikakati ya kukuza maadili kwa watumishi wa Sekta ya
Umma na watu binafsi, wananchi bado wamekuwa wakilalamika kuwepo
urasimu usio wa lazima wenye lengo la kutengeneza mazingira ya rushwa na
huduma zisizoridhisha. Aidha, wapo baadhi ya wafanyabishara binafsi
wasiozingatia maadili na hata kufikia hatua ya kuchochea utoaji wa
rushwa au kuzalisha bidhaa zisizo na viwango.
Katika jitihada za kuhakikisha
kwamba watumishi wa Umma wanakuwa waadilifu na wanafuata maadili mema,
Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete
ilibuni mikakati ya kuwa na utaratibu mpya kwa viongozi na watumishi wa
Sekta za Umma na Binafsi kusaini Ahadi ya Uadilifu (integrity pledge).
Ahadi ya Uadilifu ni tamko
rasmi na bayana la dhamira ya kuwa na mwenendo wa kimaadili na kuunga
mkono kampeni ya kitaifa ya maadili na mapambano dhidi ya rushwa. Kwa
kusaini tamko hilo, mhusika au taasisi inakuwa imejipambanua kwa Umma
kuwa haitajiingiza katika masuala yasiyo ya kimaadili katika utoaji
huduma na uendeshaji wa biashara.
Kwa mujibu wa Kamishina wa
Maadili Jaji Salome Kaganda, kuna aina tatu za hati za Ahadi ya Uadilifu
yaani; Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma, Watumishi wa Umma na
Sekta binafsi ili kila kundi liwajibike kwa namna yake.
Akizindua Hati za Uadilifu
mwezi agosti 2015, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema, kuwepo kwa Hati
hizo ni hatua kubwa muhimu na ya kihistoria katika safari ya kuboresha
na kuhuisha mifumo ya uadilifu iliyopo ili iweze kwenda sambamba na
mazingira na nyakati zilizopo.
Dkt. Kikwete hakusita kuelezea
chimbuko la Hati ya Madili kwa kusema, “Kwa muda mrefu kumekuwepo na
changamoto kubwa katika kupambana na rushwa kama moja ya tatizo kubwa la
utovu wa uadilifu nchini.
Tumechukua hatua kadhaa ikiwemo
kutengeneza Mkakati wa Mapambano Dhidi ya Rushwa na mabadiliko katika
Sheria ambayo ilisaidia kuanzishwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU). Tumepata mafanikio makubwa na ya kutia moyo ingawa
bado zipo changamoto na manung’uniko ambayo hatuwezi kuyapuuza.”
Dkt. Kikwete alifafanua kuwa,
kwa madhumuni ya kuyaongezea mapambano haya nguvu na kasi, Serikali
iliamua Mpango wa Mapambano dhidi ya Rushwa uingizwe katika Mpango wa
Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ili kutoa msukumo wa pekee
katika utekelezaji wake.
Akielezea juu ya Mpango wa
Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Mkurugenzi Mtendaji wa BRN Bw.
Omar Issa alisema kuwa Ahadi ya Uadilifu ni moja ya maeneo 12 yaliyo
katika Mpango wa Mapambano dhidi ya Rushwa chini ya Mpango wa Tekeleza
kwa Matokeo Makubwa sasa (BRN).
Kwa mujibu wa Mkurugenzi
Mtendaji huyo, matokeo ya utafiti uliofanywa katika kutekeleza mpango
huo imeonekana kwamba moja ya changamoto iliyoonekana katika eneo la
utoaji huduma na uendeshaji biashara nchini ni tatizo la rushwa na utovu
wa maadili katika taasisi za umma na binafsi. Hivyo kulikuwa na haja ya
kuweka mikakati ya uwajibikali na kufuata maadili katika utumishi wa
Umma na Sekta binafsi.
Katika kuweka msisistizo wa
suala la maadili na uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma, Rais wa Awamu ya
Tano Dkt. John Pombe Magufuli ametoa agizo kwa watumishi wote wa umma
kujaza Hati ya Ahadi ya Uadilifu (integrity pledge) ambayo imeeleza wazi
masharti ya namna mtumishi wa Umma anavyopaswa kufanya kazi.
Lengo ni kusaidia kukuza
maadili na mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa katika Sekta ya Umma na
binafsi kwa kuwa ahadi au tamko hilo linashawishi viongozi, watumishi
wa Umma na Makampuni binafsi kuwa tayari kufanya kazi kwa kufuata
misingi ya maadili na kupambana na rushwa kwa hiari yao wenyewe.
Akiunga mkono juhudi za Dkt.
Magufuli katika kusimamia nidhamu kwa Watumishi wa Umma, aliyekuwa
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kwamba Hati ya Uadilifu
(integrity pledge) itakuwa chachu ya harakati za kukuza uadilifu na
mapambano dhidi ya rushwa nchini. “Ahadi ya uadilifu itaweka kauli
thabiti ya kimaadili ambayo itaonyesha nia ya kutekeleza majukumu ya
viongozi na watumishi wa umma,” alisisitiza Balozi Sefue.
Alifafanua kuwa, ujazaji wa
Hati hiyo hiyo utakuza utamaduni wa viongozi, watumishi wa Umma na Sekta
binafsi kwa ujumla kuwa tayari kufanya kazi kwa kufuata misingi ya
maadili na kupambana na rushwa kwa hiari yao.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Utumishi na Utawala Bora Bi. Angela Kairuki amesema kwamba
mtumishi wa umma anatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu na
uadilifu bila kutoka nje ya mstari.
Mara baada ya kuapishwa kuwa
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw Agrey Mwanri amesema atasimamia ipasavyo
maadili ya utumishi wa Umma hususan katika kutekeleza miradi ya
maendeleo katika mkoa wake huku akiahidi kuwawajibisha watumishi
watakaokiuka maadili ya utumishi wa umma.
Tangu achaguliwe kuwa Rais wa
Serikali ya Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli amewachukulia hatua
baadhi ya viongozi wa Umma kwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa
majukumu waliyopewa. Viongozi hao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Uchukuzi, Dkt. Shaaban Mwinjaka, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari,
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mapato, Mkurugenzi wa Vitambulisho vya Taifa na
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Dkt.
|
May 16, 2016
MAADILI NI MSINGI WA UWAJIBIKAJI KATIKA UTUMISHI WA UMMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment