Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watanzania Waishio nchini
Uingereza kwenye ubalozi wa Tanzania uliopo London Mei 14, 2014.
Kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki
Kikanda na Kimataifa, Augustine Mahiga. Kushoto ni KaimuBalozi wa
Tanzania nchini Uingereza, Msafiri Marwa .
………………………………………………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imeamua kupambana na wala rushwa ili kiasi kidogo cha
rasilmali kilicholengwa kiweze kuwafikia wananchi.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi,
Mei 14, 2016) wakati akizungumza na Watanzania waishio Uingereza kwenye
mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini London,
Uingereza.
“Jambo tuliloamua kuanza nalo ni
kupambana na rushwa. Tumeamua kufanya hivyo ili kurudisha umoja na
maelewano miongoni mwa Watanzania, tunataka tuibadili Tanzania ili iwe
ni ya Watanzania wote… tumechoka kuambiwa sehemu fulani mradi
umekamilika halafu ukienda kuangalia hukuti kitu na fedha ile haipo,”
alisema huku akishangiliwa.
Akizungumzia zoezi la kusaka
watumishi hewa, Waziri Mkuu alisema Serikali itawashughulikia wale wote
waliohusika na zoezi hilo. “Wafanyakazi hewa wamefikia zaidi ya 10,000
na tumeokoa zaidi ya sh. bilioni 4.5 zilizokuwa zikipotea kila mwezi.
Tukikamilisha zoezi la kusaka watumishi hewa, sasa tutataka kujua ni
akina nani walikuwa wakipokea fedha hizo. Waliohusika tutashughulika
nao,” alisisitiza.
Alisema hivi sasa Serikali
inalenga kuwa na watumishi ambao wanafanya kazi kwa uaminifu, uadilifu
na uwajibikaji mahali pa kazi. “Hiki ndicho kipaumbele cha Serikali ya
awamu ya tano na tena zoezi hili litakuwa endelevu”, alisema Waziri
Mkuu.
Akizungumzia kuhusu ukuaji wa
uchumi, Waziri Mkuu ambaye alikuwa London kuhudhuria mkutano uliojadili
mapambano dhidi ya rushwa kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli,
alisema lengo la Serikali hivi sasa ni kuona kuna ukuaji wa uchumi
unaoenda sambamba na huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Alisema viwanda vingi viliuzwa na
watu waliovinunua wakageuza kuwa ni maghala ya kufugia wanyama. Sisi
tunataka vifufuliwe ili teknolojia mpya na za kisasa zije Tanzania.
Nafasi ya kuwekeza iko kwa Watanzania wote walioko nyumbani na ninyi
mlioko nje,” alisema.
Alisema ardhi ipo ya kutosha na
akawataka wawaalike marafiki zao waje kuwekeza nchini, ili mradi wawe ni
watu makini, wenye nia ya dhati ya kuwekeza nchini na wenye mitaji na
siyo madalali (middlemen). “Tunataka usindikaji wa mazao na bidhaa
ufanyike nchini mwetu badala ya kupeleka mazao ghafi nje ya nchi, kwa
njia hiyo tutakuwa pia tumezalisha ajira kwa watu wetu,” alisema.
“Kuna Watanzania wanaishi
Botswana, Ujerumani na Poland wameshaleta wawekezaji nchini. Kwa mfano
wa Poland wameleta mradi wa umeme katika vijiji vitani wilayani Ileje.
Kwa hiyo ninyi endeleeni kuishi Uingereza lakini mhakikishe kuwa ukaaji
wenu hapa, unaleta tija kule nyumbani. Kumbukeni Tanzania na muwe tayari
kuihudumia Tanzania,” alisema.
“Serikali inaamini itanufaika na
uwepo wenu hapa Uingereza. Muweke kipaumbele cha kuwekeza nyumbani na
mkishindwa mtutafutie marafiki zenu. Mwenye uwezo andaa andiko la mradi
halafu uwasiliane na Balozi ili akusaidie kutafuta wahusika kule
nyumbani,” aliwaasa.
Akijibu swali kuwa ana maoni gani
juu ya Bunge kutorushwa ‘LIVE’, Waziri Mkuu alisema hatua hiyo
ilichukuliwa ili kuwawezesha watu kufanya kazi kama ambavyo kaulimbiu ya
Mhe. Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu inavyosema.
“Bunge la Tanzania lilikuwa ni
bunge pekee katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na duniani ambalo
lilikuwa likirushwa LIVE kuanzia asubuhi hadi usiku. Ina maana katika
kipindi cha Bunge la bajeti, ambalo linaendeshwa kila siku kwa miezi
mitatu, Watanzania nao wangekuwa LIVE kwa miezi mitatu,” alisema.
“Tulilazimika kujifunza kutoka
kwenye mabunge mengine. Hivi hapa Uingereza mnaangalia Bunge live kila
siku?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa kuwa linarushwa LIVE kwa pipindi
kisichozidi dakika 15 wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu tu.
Akitoa ufafanuzi, aliwaeleza
kwamba Bunge la Tanzania linarusha ‘LIVE’ kila siku asubuhi wakati wa
maswali ya kawaida na Alhamisi asubuhi wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu
lakini mijadala yote hurekodiwa na kuhaririwa na kisha kurushwa kuanzia
saa 8-9 mchana na saa 3-4 usiku kwa siku husika.
Kwa Watanzania wanaopenda kufanya
kazi na wanapenda kufuatilia mambo ya Bungeni, walikuwa hawaoni LIVE
coverage jwa sababu walikuwa kazini lakini sasa hivi wanaweza kufuatilia
masuala ya bunge kwani muda wa jioni uliopangwa mtu anakuwa ametoka
kazini na anaweza kuangalia televisheni akiwa nyumbani baada ya kutoka
kazini


No comments:
Post a Comment