![]() |
Ofisi ya Taifa ya Takwimu
imetangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Aprili 2016 na kusema kuwa
umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 5.1 kutoka asilimia 5.4
iliyokuwepo mwezi Machi, 2016.
Hii
inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma kwa
mwezi Aprili 2016 imepungua kidogo ikilinganishwa na kasi ya upandaji wa
bei ya bidhaa na huduma iliyokuwepo mwezi Machi mwaka huu.
Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
Bw. Ephraim Kwesigabo ametoa taarifa hiyo jana jijini Dar es salaam na
kueleza kuwa kupungua kwa mfumuko huo kumesababishwa na kupungua kwa
kasi ya bei ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula katika
maeneo mbalimbali nchini.
Alisema
Takwimu zilizokusanywa katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwenye bidhaa
zinazotumika kupima mfumuko wa bei kwa mwezi Aprili 2016 zimeainisha
kuwa bidhaa zisizo za vyakula katika soko zikiwemo Gesi , dizeli na
mafuta ya taa zimechangia kupungua kwa mfumuko huo.
Alisema
kuwa pamoja na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa hizo kwa
mwezi Aprili 2016, baadhi ya bidhaa za vyakula ikiwemo mchele, unga wa
Mahindi na mkaa ilionyesha kuongezeka katika kipindi hicho.
Akizungumzia
Kuhusu Fahirisi za Bei ambacho ni kipimo kinachotumika kupima
mabadiliko ya bei ya bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya binafsi hapa
Tanzania kwa mwezi Machi na Aprili Bw. Kwesigabo alisema kuwa
zimeongezeka hadi kufikia 102.46 kutoka 101:93 za mwezi Aprili.
Alisema
kuwa tofauti na mwezi Machi bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka
kwa fahirisi kwa mwezi Aprili ni unga wa muhogo, dagaa, choroko, maziwa
ya ungana na matunda aina ya machungwa.
Aidha,bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi za bei ni pamoja na mvinyo, bia kuni na mazulia.
Kwa
upande wa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na
huduma za mlaji kwa mwezi Aprili, 2016 umefikia shilingi 97 na senti 60
ikilinganishwa na uwezo wa shilingi 98 na senti 11 wa mwezi Machi 2016.
“Uwezo
wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma zilezile
kwa mlaji kwa mwezi Aprili 2016 umepungua, hii ina maana kuwa sasa mtu
anahitaji kuongeza ya shilingi 2.40 ili aweze kununua bidhaa na huduma
sawa na zile alizokuwa na uwezo wa kuzinunua mwezi Machi ” Alisema Kwesigabo.
|
![]() |
| Mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Prof. Haji Semboja akifafanua kwa waandishi wa Habari kuhusu mwenendo wa uchumi wa Tanzania |




No comments:
Post a Comment