![]() |
| NAIBU Waziri, Wizara ya Fedha na
Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameliambia Bunge Mjini Dodoma, leo tarehe
12 Mei, 2016, kwamba serikali inaandaa sera ya Taifa ya huduma ndogo za
fedha ya mwaka 2016, itakayosimamia na kutatua changamoto zinazoikabili
sekta hiyo
Alisema kuwa sera hiyo
itawasilishwa mbele ya Baraza la Mawaziri hivi karibuni kabla ya
kupelekwa bungeni hatimaye itapatikana sheria ya kusimamia taasisi ndogo
za fedha-microfinance Act, 2016.
“Serikali inatambua changamoto ya
taasisi binafsi za fedha zinazosumbua wananchi, hivyo sheria hiyo
ikitungwa itasaidia kuondoa matatizo hayo” alisisitiza Dkt. Kijaji
Naibu Waziri huyo wa Fedha na
Mipango alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mhe. Rahisa Abdalah Musa
(Viti maalumu), aliyetaka kujua serikali ilikuwa na mpango gani wa
kudhibiti utitiri wa taasisi za fedha pamoja na mabenki ili yalete tija
kwa Taifa kwa kuwakopesha wananchi
Akijibu swali la msingi na
maswali ya nyongeza yaliyoulizwa na Mhe. Faida Mohamed Bakar (Viti
maalumu) aliyetaka kujua mikakati ya serikali ya kuanzisha benki ya
wafanyabiashara wakubwa na wadogo ili kuwawezesha kupata huduma bora,
Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa serikali haina mpango wowote wa kufanya
hivyo.
Alisema kuwa badala yake serikali
inafanya jitihada za kuimarisha benki zake zilizopo ikiwemo Benki ya
maendeleo ya Kilimo (TADB) na Benki ya Rasilimali (TIB) ili kukidhi
mahitaji ya wafanyabiashara wa kada mbalimbali.
“Serikali imeiboresha kimuundo,
Benki ya Rasilimali (TIB) kwa kuunda kampuni tatu zinazofanyakazi kwa
kujitegemea lakini kwa ushirikiano wa karibu” alisisitiza Dkt. Kijaji
Alizitaja kampuni hizo kuwa ni
TIB Benki ya Maendeleo itakayotoa mikopo ya muda wa kati na mrefu kwa
wafanyabiashara wakubwa na wa kati, TIB Benki ya Biashara
itakayowahudumia wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo na TIB
Rasilimali itakayohusika na masuala ya ushauri kwenye Soko la Hisa na
Mitaji la Dar es salaam
“Pamoja na mambo mengine, kampuni
hii inawajibika kuwashauri wafanyabiashara, hususan wa sekta ndogo ya
fedha kupata mitaji kupitia Soko la Hisa la Dar es salaam” aliongeza
Dkt. Kijaji
Dkt. Kijaji alisema kuwa pamoja
na juhudi za serikali za kuboresha benki hizo, ikiwemo Benki ya Posta,
Serikali kupitia Benki Kuu (BOT) inaendelea kuweka mazingira wezeshi
ikiwemo kutunga sheria, kanuni na taratibu za kusaidia nguvu za wananchi
na sekta binafsi kuanzisha benki au taasisi za fedha katika maeneo yao
“Ni matarajio yetu kuwa wananchi
wanatumia fursa ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini
kuwekeza wao wenyewe au kuzishawishi benki za biashara kuanzisha huduma
za kibenki katika maeneo yao” alisema Dkt. Kijaji
Kuhusu ombi la mbunge huyo
kuitaka serikali iingilie kati masuara ya riba zinazotozwa na taasisi za
fedha na kuwaumiza wananchi, Dkt. Kijaji alisema kuwa serikali haiwezi
kudhibiti wala kuingilia jambo hilo.
Alisema kuwa Serikali ilijitoa
katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kifedha tangu mwaka
1991 ili kuruhusu ushindani huru na kuboresha huduma katika sekta ya
fedha hivyo viwango vya riba na mikopo vinavyotozwa na benki hizo na
taasisi nyingine za fedha zinapangwa kutokana na nguvu ya soko.
Dkt Kijaji alieleza kuwa katika
upangaji wa viwango vya tozo na riba mbalimbali benki na taasisi za
fedha huzingatia gharanma za upatikanaji wa fedha, halikadhalika gharama
za uendeshaji na sifa alizonazo mkopaji”Alisisitiza Dkt Kijaji
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
DODOMA
12/5/2016
|
May 13, 2016
SERIKALI KUTUNGA SERA YA KUSIMAMIA SEKTA NDOGO YA FEDHA NCHINI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment