ZAITUNI KIBWANA NA ZAINAB IDDY
BILIONEA maarufu Afrika, Mnigeria Aliko Dangote, amejikuta akiwa
vitani na mfanyabiashara maarufu hapa nchini ambaye ni Mwenyekiti wa
Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, katika suala zima la kuimiliki klabu ya soka ya Yanga.
Wawili hao wamejikuta wakiwa na nafasi kubwa ya kufanikisha azma yao
hiyo baada ya bilionea aliyekuwa akiibeba Yanga kwa muda mrefu, kuamua
kuachia ngazi.
Habari zilizozagaa kwenye mitandao Dar es Salaam jana na
kuthibitishwa na mmoja wa wanachama maarufu wa klabu hiyo, Jerry Muro,
zinasema kuwa bosi huyo amefikia uamuzi huo ikiwamo kujiuzulu nafasi
yake ya uongozi kutokana na kile alichosisitiza ‘imetosha’.
Na habari zaidi zinadai kuwa Mengi ameonyesha nia kitendo kilichowafanya baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wakiwamo wazee wao, kupanga kumfuata kumtaka afanye hivyo.
Na iwapo Mengi atakubali, ni wazi atakuwa na kazi kubwa ya kushindana
na Dangote aliyezaliwa Aprili 10, 1957 anayemiliki Kampuni ya Dangote
Group, inayoendesha biashara zake katika nchi mbalimbali za Afrika
zikiwamo Benin, Ethiopia, Senegal, Cameroon, Ghana, Afrika Kusini, Togo,
Tanzania na Zambia.
Mnigeria huyo anatajwa kuwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni
14.9 sawa na Sh trilioni 32.5, akitajwa kushika nafasi ya 67 katika
orodha ya matajiri duniani, huku akiwa wa kwanza Afrika.
Na iwapo mmoja wa wawili hao atafanikiwa kuitwaa Yanga, ni wazi kuwa
klabu hiyo itakuwa haijapoteza chochote baada ya kujiuzulu kwa bilionea
wao.
Juu ya kujiuzulu kwa bosi huyo wa Yanga, imedaiwa kuwa kumetokana na
kuchoshwa na shutuma zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali na
wengine kutoka ndani ya klabu hiyo ambao wanatumiwa na baadhi ya
wafanyabiashara kwa masilahi yao binafsi.
Mbali na taarifa hizo, chanzo cha ndani ya Yanga, kimeliambia BINGWA
kuwa kiongozi huyo mara kwa mara amekuwa akiumizwa na tabia za baadhi ya
watu ndani ya timu hiyo hususani wanachama kumtukana na kumkebehi kwa
hatua yake ya kutaka kuimiliki timu.
“Suala la kujiuzulu ni kweli na hii inatokana na baadhi yetu
wanachama kufanya mambo anayoona kama anadharauliwa na kudhihakiwa,
hivyo ameona bora akae pembeni ili kulinda heshima yake.
“Tangu jambo hilo kuibuka mchana huu (jana), viongozi wa Yanga
wamekuwa wakihaha kufanya mawasiliano naye, lakini pia wakipishana
katika ofisi yake ili kumsihi asitangaze uamuzi huo,” alisema.
Chanzo chetu hicho kilizidi kupasha: “Tayari wazee wameshakubaliana
leo (jana) jioni kukaa na Mengi ili kuona jinsi watakavyoweza kuisaidia
Yanga mara tu bilionea wao atakapotangaza rasmi uamuzi wake huo.”
BINGWA lilimtafuta Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit,
ambapo alisema taarifa hizo amezisikia, lakini hawezi kuzungumzia hadi
awe na uhakika juu ya jambo hilo.
“Hizi taarifa na mimi nimezisikia pia, lakini siwezi kuzungumzia
lolote kwani sijapata taarifa maalumu juu ya jambo hilo, zinaweza kuwa
kweli au si kweli,” alisema.
Ujio wa Dangote au Mengi ndani ya Yanga, utaifanya klabu hiyo
kuendelea kuwa tishio nchini na Afrika kwani haitakuwa na shida kama
ilivyokuwa kwa kipindi chote chini ya bilionea wao aliyedaiwa kutangaza
kujiondoa Jangwani jana.
Katika hatua nyingine, wanachama na mashabiki wa Yanga jana
walifurika makao makuu ya klabu hiyo katika kile kinachoonekana
kutokubaliana na mpango wa kujiuzulu kwa bilionea wao huyo.
BINGWA lilifika katika jengo lao lililopo makutano ya Mtaa wa Twiga
na Jangwani, Dar es Salaam na kukuta umati wa mashabiki wa Yanga
waliokuwa wakiwashutumu baadhi ya viongozi wao kwa kile walichodai wao
kuwa sababu ya kujiuzulu kwa ‘mfalme’ wao huyo ambapo waliwaonya kufanya
kile kinachowezekana kuinusuru klabu yao.Chanzo Bingwa.



No comments:
Post a Comment