![]() |
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Vyama vya michezo nchini
vimeaswa kuthamini na kutoa shukrani baada ya kumaliza mashindano kwa
lengo la kuimarisha ushirikiano pamoja na kuwapa moyo wanamichezo na
wadhamini wa mashindano.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu
wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja wakati wa hafla ya
kukabidhi zawadi na vyeti kwa washiriki, wadhamini na waandishi wa
habari waliofanya vizuri katika kupiga picha na kuandika habari za
Mashindano ya Magari yaliyofanyika Julai 8 hadi 10 wilaya ya Bagamoyo
mkoani Pwani na kusimamiwa na Taasisi ya Automobile Association Tanzania
(AATanzania).
“Vyama vingine vya michezo
nchini vinapaswa kuiga mfano wa AATanzania wa kutoa shukrani baada ya
mashindano, hili ni fundisho kubwa, wanapaswa kuthamini na kutambua
msaada wa kufanikisha mashindano yeyote wanayoyaandaa” alisema Kiganja.
Katibu huyo aliongeza kuwa,
yanafanyika mashindano ya michezo mbalimbali nchini yakiwa lengo la
kuburudisha na kuelimisha jamii, ni wajibu wao kuiga mfano uliouoneshwa
na AATanzania wa kutoa shukrani baada ya mashindano.
Naye Rais wa AATanzania Bw.
Nizar Javan ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na BMT ambao
wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mashindano hayo
yaliyofanikiwa kwa ufanisi mkubwa.
Bw. Nizar aliongeza kuwa
mashindano hayo yaliisha salama bila ya kutokea ajali yeyote hatua
ambayo inaendana na kauli mbiu yao inayosema “Usalama kwanza”.
Kwa upande wa Jeshi la Polisi,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Afisa Mnadhimu Kikosi cha
Usalama Barabarani (SACP) Fortunatus Musilimu amewashukuru AATanzania
kusimamia, kuandaa na kufanikisha mashindano hayo ambayo yamezingatia
usalama wa washiriki wa mashindano na magari yaliyotumika.
Katika kuitangaza Tanzania
kupitia mchezo wa magari, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO)
Zamaradi Kawawa amewasihi waandaaji wa mashindano hayo kuebdelea
kuhamasisha wachezaji wa mchezo huo kujitokeza kwa wingi na kushiriki
mashindano hayo, hatua ambayo itasaidia kuongeza ushindani na kuitangaza
Tanzania Kimataifa kwa kuwa mchezo huo unashirikisha mataifa malimbali.
Waandishi wa habari waliopata
vyeti na zawadi kwa kuuhabarisha umma juu ya mashindano hayo ni pamoja
na Mohamed Ugassa kutoka gazeti la The Guardian, Jimmy Tara wa ITV,
Brown Msyani kutoka gazeti la Citizen, Timzoo Kalugira na Michael Maluwe
kutoka Azam Tv, Nasongelya Kilyinga gazeti la Daily News na Miguel
Suleyman ambaye ni wandishi wa habari wa kujitegemea.
Pamoja na waandishi hao, wadau
waliopewa zawadi kwa kutambua mchango wao katika kufanikisha mashindano
hayo ni Jeshi la Polisi, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Baraza la Michezo Tanzania na Hoteli ya Southern Sun.
Mashindano hayo ya magari
yaliyofanyika nchini yanatambuliwa na Shirikisho la Michezo ya Magari
Duniani (FiA) ambayo AATanzania ni mwanachama.
|
August 16, 2016
VYAMA VYA MICHEZO NCHINI VIMEASWA KUIGA MFANO WA AATANZANIA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment