MSAJILI
wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ameitisha Baraza la Vyama vya
Siasa ili kunusuru mvutano uliojitokeza kati ya Jeshi la Polisi na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Jaji
Mtungi amevitaka vyama vya siasa vilivyotangaza kufanya maandamano na
mikutano isiyo na tija nchi nzima kuacha, badala yake warudi kwenye meza
ya mazungumzo ili kuondoa tofauti zinazojitokeza.
Kauli
ya Jaji Mutungi imekuja baada ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM) nao kutangaza maandamano ya amani kwa ajili ya kupongeza
utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli, huku Chadema kikiitisha
maandamano na mikutano isiyo na kikomo nchi nzima, ambayo imepewa jina
la Operesheni Ukuta.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Jaji Mutungi alisema
kufanyika kwa maandamano na mikutano hiyo, hakuwezi kuondoa changamoto
za kisiasa zilizopo, hivyo basi wanapaswa kukaa kwenye meza moja kwa
ajili ya kujadili tofauti zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.
“Ninawaomba
wale wote wenye lengo la kuitisha maandamano na mikutano ya kisiasa
kuacha kwa sababu haiwezi kusaidia kuondoa changamoto zilizopo, bali
tunapaswa kukaa kwenye meza moja ya mazungumzo ili tuweze kujadili
tofauti hizo na kuzipatia majibu,” alisema Jaji Mutungi.
Aliongeza
kuwa licha ya kuwapo kwa jitihada za viongozi mbalimbali kujadili suala
hilo, lakini vyama hivyo vimeonekana bado vikiendelea na misimamo yao
ya kuitisha mikutano na maandamano yasiyo na kikomo, jambo ambao
linaweza kuleta hofu kwa wananchi.
Jaji
Mutungi alisema katika kipindi hiki ambacho wananchi wametulia, hakuna
haja ya kuwatia hofu au wasiwasi ili ionekane kuwa nchi ina ombwe kubwa
la uongozi, jambo ambalo linaweza kurudisha nyuma juhudi za kuleta
maendeleo.
No comments:
Post a Comment