
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J.
Kairuki (Mb) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawako pichani)
kuhusu utekelezaji wa agizo la kuondoa watumishi hewa katika orodha ya
malipo ya mishahara Serikalini ofisini kwake mapema leo.

Baadhi ya waandishi wa habari
wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) alipozungumza leo
ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………………………
Hussein Makame-MAELEZO
Waajiri 264 kati ya waajiri wote
409 Serikalini wamewasilisha taarifa zao kuhusu kuwepo kwa watumishi
hewa ambapo kati ya waajiri hao waajiri 63 wamethibitisha kwamba hawana
watumishi hewa katika Taasisi zao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi Wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki
(MB), amebainisha hayo wakati alipozungumzia na waandishi wa habari
ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa waajiri 201 wana
watumishi hewa kuanzia mmoja na kuendelea.
“Waajiri 264 kati ya waajiri wote
409 wamewasilisha taarifa zao kuhusu uwepo wa watumishi hewa. Kati ya
waajiri 264 waliowasilisha taarifa zao, waajiri 63 wamethibitisha kwamba
hawana watumishi hewa katika Taasisi zao na waajiri 201 wana watumishi
hewa mmoja (1) na kuendelea.” Alisema Waziri Kairuki.
Hata hivyo, alisema zipo taasisi
145 ambazo hazijawasilisha taarifa iwapo zina watumishi hewa au la
ikiwemo Mabaraza 11, Bodi 10, Vyuo Vikuu 25, Hospitali 3 na Ofisi za
Makatibu Tawala wa Mikoa 12.
Alizitaja taasisi nyingine kuwa ni
Mamlaka 6, Tume 10, Mamlaka za Serikali za Mitaa 38, Taasisi za
Umma na Wakala 30 ambapo aliziagiza Taasisi zote ambazo hazijawasilisha
taarifa za watumishi hewa kufanya hivyo kabla au ifikapo tarehe 26
Agosti mwaka huu.
Waziri Kairuki alieleza kuwa
kuanzia Agosti 15 mwaka huu, ofisi yake ilianza zoezi la uhakiki wa
kushtukiza katika taasisi sabini za Serikali zikiwepo Wizara, Idara za
Serikali Zinazojitegemea na kwamba zoezi hilo linaendelea.
Aliongeza kuwa uhakiki wa
kustukiza utafanyika pia kwenye Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za
Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma kwa madhumuni ya kujiridhisha
kwamba taarifa za watumishi hewa zilizowasilishwa na waajiri ni sahihi.
Alibainisha kuwa katika
kufanikisha uhakiki huo, Ofisi yake imechukua hatua kadhaa ikiwemo
kuendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Maafisa Utumishi wenye
dhamana ya kutumia mfumo wa malipo ya mshahara kukuza uwajibikaji kwa
maafisa wanaosimamia malipo ya mishahara kwa kuwachukulia hatua za
kinidhamu au kisheria wanaobainika kusababisha watumishi hewa.
“Aidha ofisi yangu pia inafanya
uhakiki wa kushtukiza na kuanza safari ya kuunganisha Mfumo wa Malipo ya
Mishahara na mifumo mingine mikubwa kama ya NIDA, RITA na Baraza la
Mitihani la Taifa, na kuwezesha mfumo kuwaondoa moja kwa moja
(automatically) watumishi waliofikisha umri wa kustaafu kwa lazima.”
alisema.
Waziri Kairuki atatoa taarifa
kamili ya watumishi hewa baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa waajiri
ambao hawajawasilisha taarifa hizo na kukamilika kwa zoezi la uhakiki
wa Taasisi sabini (70) linaloendelea sasa.
“Hivyo naagiza Taasisi zote ambazo
hazijawasilisha Taarifa za Watumishi Hewa kufanya hivyo kabla au
ifikapo tarehe 26 Agosti, 2016.” Alisema Waziri Kairuki.
Alisema kuwa ofisi yake
itawasilisha taarifa rasmi ya watumishi hewa kwa Mheshimiwa Rais ikiwa
na orodha na majina ya Taasisi ambazo zimewasilisha taarifa ya watumishi
hewa na na zile ambazo hazijawasilisha taarifa hizo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli mnamo Machi 15 mwaka huu aliwaagiza
Wakuu wa Mikoa na Waajiri wote kwa ujumla kuchukua hatua ya kuhakikisha
katika Mikoa au Taasisi zao hakuna watumishi hewa ifikapo tarehe 30
Machi, 2016.
Katika kutekeleza agizo hilo Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekuwa
ikifuatilia utekelezaji wa agizo hilo na mnamo Mei 26 mwaka huu waajiri
wote waliagizwa kuwasilisha taarifa za mwisho za zoezi la kuwabaini na
kuwaondoa watumishi hewa katika orodha za malipo ya mshahara (payroll)
ifikapo mwisho wa Mwezi Juni, 2016.
Waajiri walitakiwa kutuma jina la
Taasisi, Fungu la Taasisi (Vote), namba ya Utambulisho ya Mtumishi wa
Umma (Cheki Namba), jina kamili la mtumishi; cheo cha mtumishi, jina la
tawi la Benki ambalo mshahara wa mtumishi umekuwa ukipitishwa au
ukilipwa.
Taarifa nyingine zinazotakiwa
kutumwa ni hatua zilizochukuliwa na mwajiri dhidi ya watumishi hewa
waliobainika kama kurejesha fedha, na Maafisa wengine wa Taasisi husika
waliosababisha uwepo wa Watumishi hao kuwachukulia wahusika hatua za
kinidhamu au kisheria.
Nyingine ni namba ya akaunti ya
Benki ya mtumishi, tarehe ambayo mtumishi aliondolewa kwenye mfumo wa
taarifa ya Kiutumishi na Mshahara, kiasi cha fedha zilizolipwa kwa
mtumishi husika tangu alipotakiwa kuondolewa hadi tarehe aliyoondolewa
kwenye mfumo na sababu ya kuondolewa kama utoro, kufariki dunia, kuacha
kazi, kustaafu na sababu nyingine.
No comments:
Post a Comment