Mtandao wa Watetezi wa Waki za Binadamu (THRDC) kwa niaba ya wanachama
wake tunalani vikali maujai ya askari wa jeshi la polisi huku
tukisisitiza kwamba askari wa jeshi la polisi wanaofanya kazi katika
misingi na sheria ni watetezi wa haki za binadamu kama walivyo watetezi
wengine.
Kutokana na taarifa rasmi ya jeshi la polisi ni kwamba
mnamo tarehe 23/08/2016 saa moja usiku maeneo ya Mbagala Mbande kata ya
Mbande Temeke, majambazi ambao idadi yao haikuweza kufahamika wakiwa na
silaha za moto walivamia benki ya CRDB tawi la Mbande ambapo
waliwashambulia na kuwaua askari wanne wa Jeshi la Polisi waliokuwa
kazini na kuwajeruhi raia wawili waliokuwa jirani na eneo hilo.
Askari waliofariki katika tukio hilo ni E,5761 CPL Yahaya, F,4660 CPL
Hatibu, G9524 PC Tito na G.9996 PC Gastone na raia waliojeruhiwa ni Ally
Chiponda na Azizi Yahaya wote wakazi wa Mbande.
Katika tukio hilo,
majambazi hayo yalifanikiwa kupora silaha mbili za SMG na risasi sitini
(60) na hakuna pesa au mali za benki iliyoibiwa, ni dhahiri kwamba
walikuwa na kusudio la kujipatia silaha kwa ajili ya kufanya uhalifu na
si vinginevyo kama baadhi walivyotaka kupotosha.
Ikumbukwe kuwa
majambazi mara kadhaa mwaka jana katika maeneo mbalimbali chini, mfano
Kituo cha Stakishari Dar es Salaam na Kituo cha Polisi Ikwiriri ,
vilivyamiwa na majambazi kwa lengo la kuchukua silaha kwa ajili ya
uhalifu.
Aidha, Tunalipongoza Jeshi la Polisi kwa kuweza kuwafikia
majambazi hao huko Mkuranga bila kuumiza raia. Pia tunatoa pole kwa
familia za askari wote watano waliopoteza maisha wakiwa kazini.
Askari
anaekamilsha idadi ya askari waliouwawa kufika watano ni Askari Thomas
Njiku,Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Ujambazi alieuwa Vikindu wilayani
Mkuranga wakati akiongoza kikosi maalum cha kuwasaka watu waliosadikiwa
kuwa ni majambazi waliotekeleza tukio la kihalifu la Mbade,Mbagala.
Tunawasihi Watanzania kutoipokea dhana inayotaka kujengwa na wanasiasa
kuwa hatukemei matukio haya dhidi ya polisi.
Kumbukeni kuwa Mtandao wa
Watetezi umekuwa ukitoa matamko mbali mbali kukemea mauaji ya askari
wa jeshi la polisi, na tumekuwa mara kwa mara tukisisitiza kwamba askari
wa jeshi la polisi ni watetezi wa haki za binadamu, kwa kuwa jukumu lao
la kwanza ni kulinda mali za watu na usalama wa binadamu.
Mtandao
unatambua kuwa askari wa jeshi la polisi pia ni ndugu zetu, kaka zetu na
baba zetu hivyo madhila wanayokumbana nayo ni yetu sote.
Mfano,
katika repoti ya hali ya watetezi wa haki za binadamu kwa mwaka
jana(2015) , Mtandao uliweza kuwa na kipengele maalumu kilichozungumzia
haki za polisi na hali ya usalama kwa polisi wakiwa kama watetezi wa
haki za binadamu.
Katika ukarasa wa 18 wa repoti hiyo Mtandao uliweza
kurekodi matukio ya uvamizi na mauaji ya jeshi la polisi zaidi ya kumi
(10) na wengine watano (5) wakiachwa wamejeruhiwa. Kwa maana hii tukio
lilitokea Mbagala ni muendelezo wa matukio ya kiuhalifu yanayoendelea
nchini.
Kumekuwa na changamoto kutoka kwa Jamii kuwatambua askari
wa jeshi la polisi kama watetezi wa haki za binadamu, na hii ni kutokana
na ukweli kwamba baadhi ya askari wamekuwa wakitumia vibaya madaraka
yao kukandamiza haki za wananchi.
Hali ilivyo sasa inaweza kuharibu
dhana nzima ya polisi kuwa ni walinzi wa raia na mali zao, kwani vitendo
wanavyofanya polisi dhidi ya raia hasa wafuasi wa vyama vya siasa na
viongozi wao ni sababu kubwa ya kuharibu uhusiano mzuri kati ya polisi
na raia.
No comments:
Post a Comment