Serikali
imeagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuondoa matuta kwenye
barabara kuu, ambayo yametajwa kuwa chanzo cha ajali.
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, ametoa agizo hilo jana
wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Usalama Barabarani katika Viwanja vya
Kalangalala mkoani Geita.
Alisema
matuta yaliyoko kwenye barabara kuu, yamekuwa moja ya vyanzo vya ajali
nyingi nchini na kusisitiza kuwa hali ya ajali iliyopo ni vyema suala la
usalama barabarani kuwa ajenda ya kitaifa.
Pia
alivitaka vvyombo vya usalama, kuwachukulia hatua kali na stahiki wale
wote wanavunja sheria za Usalama Barabarani bila kumuogopa au kumuonea
mtu yeyote.
Alisema
ajali za barabarani zimekuwa ni tatizo kubwa na kuwa takwimu za miaka
mitatu kuanzia Januari 2013 hadi Desemba 2015, zinaonesha kuwa ajali
zilizotolewa taarifa ni 46,536 ambazo zimeua watu 11,230.
Masauni
alisema kuwa kundi linaloongoza kwa kuathirika na ajali hizo ni abiria
ambapo watu 3,444 wamekufa, wakifuatiwa na watembea kwa miguu 3,328.
Alisema
wapanda baiskeli wanashika nafasi ya tatu kwa watu 2,493 kupoteza
maisha, huku madereva waliokufa ni 813 na wasukuma mikokoteni zaidi ya
400 wamepoteza maisha.
“Takwimu
za miezi sita tangu Januari mpaka Agosti mwaka huu, ajali 6,971
zimetokea na kusababisha vifo 2,217 na kati ya hivyo 1,809 ni vile
vilivyotokana na pikipiki. Hali ya ajali sio nzuri na ni vyema suala la
usalama barabarani likawa ajenda ya kitaifa,” alisema.
Alisisitiza
kutolewa elimu ya watumiaji wote kuhusu matumizi sahihi ya barabara,
wamiliki na madereva kuacha kuendesha vyombo chakavu na kufanyika kwa
ukaguzi wa mara kwa mara.
“Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pia linatakiwa kuendelea kufanya ukaguzi wa matairi, bodi na vipuri vya mabasi,” alisema.
Aidha,
Masauni aliwataka watumiaji wote wa barabara, kufuata sheria na kanuni
za barabarani, kuacha kushabikia mwendo kasi, kuvuka kwenye vivuko vya
watembea kwa miguu na waendesha baiskeli na mikokoteni kuacha kuendesha
barabarani na watoto kuvuka barabara wakiwa chini ya uangalizi.
Naibu
Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ambaye pia ni
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Edwin
Ngonyani, alisema kutokana na kukithiri kwa ajali, Baraza lilikuja na
mikakati ya miezi sita ya kupunguza ajali hususan zinazotokana na makosa
ya kibinadamu.
Alisema
makosa ya kibinadamu yamekuwa yakichangia ajali kwa asilimia 80 na
kufuatiwa na mwendokasi ambao unachangia kwa asilimia 12, mazingira ya
barabara yanachangia kwa asilimia 6 na asilimia 2 zinatokana na sababu
nyingine.
“Tumekuja
na mikakati ambayo inatekelezwa kwa miezi sita, lengo kuu ni kuondoa
makosa ya kibinadamu yanayochangia ajali, na Februari mwakani
tutatathmini mafanikio ya mikakati hiyo,” alisema.
Kamanda
wa Kikosi cha Usalama Barabarani katika Jeshi la Polisi, Mohammed
Mpinga, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama
Barabarani, alisema katika Wiki ya maadhimisho hayo watoa elimu ya
matumizi sahihi ya barabara, na kutoa elimu kwa waendesha pikipiki 300
na walimu 100, na pia watakagua vyombo vya moto na kupima afya za
madereva kwa kutumia zahanati mwendo.
Mkuu
wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, ambaye pia ni Katibu wa Baraza
la Taifa la Usalama Barabarani, Naibu Kamishna, Mohamed Mpinga
akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani
inayofanyika Kitaifa katika Viwabya vya CCM Kalangalala mjini Geita.
Maadhimisho hayo yalizinduliwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani,
Mhandisi Hamad Masauni (kulia).
Mgeni
rasmi Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni
(kulia), akimsikiliza Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani kutoka
Makao Makuu, Koplo Faustina Ndunguru wakati alipokuwa anatoa maelezo
jinsi magari mbalimbali yanavyovunja sheria za barabarani. Picha zote na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mgeni
rasmi Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni
(kushoto) akimpa zawadi ya Kombe la Ushindi wa kwanza Mwanafunzi wa
Shule ya Msingi Bunge jijini Dar es Salaam, Veronica Innocent, ambaye
alishinda nafasi ya kwanza katika uchorani wa picha zinazoonyesha
usalama barabarani ambayo zilipambanishwa katika shule za Mkoa wa Dar es
Salaam na Geita.
Washiriki
wa maonesho (waendesha bodaboda) wakiwa katika maandamano ya
kuadhimisha Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani iliyozinduliwa katika
Viwanja vya CCM Kalangalala, mjini Geita jana. Kauli mbiu ya Maadhimisho
ya mwaka huu ni “Hatutaki ajali tunataka kuishi salama”.
No comments:
Post a Comment