Benki
ya Dunia inakusudia kuipatia Tanzania ruzuku na mkopo wenye masharti
nafuu wa dola Bilioni 1 nukta 6 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 3
nukta 5 kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo
nishati ya umeme, kilimo biashara na ukarabati wa miundombinu ya reli ya
kati.
Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Benno Ndulu amesema Jijini Washington
DC, Marekani ambako Ujumbe wa wataalamu wa masuala ya uchumi na Fedha
kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanashiriki mkutano wa mwaka wa Benki
ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kwamba mazungumzo kuhusu
mkopo huo yako katika hatua za mwisho.
Prof.
Ndulu amesema kuwa upatikanaji wa mkopo huo utaisaidia serikali
kuboresha miundombinu yake mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya sekta
ya viwanda kwa kuimarisha pia mazingira ya sekta binafsi
kufanyabiashara na kuwekeza mitaji na teknolojia.
“Mbali
na mkopo huo ambao ni muhimu kwa taifa, tunajadili pia namna ukuaji wa
uchumi unavyotakiwa kuakisi maisha ya kawaida ya wananchi wetu kwa
kupiga hatua kimaisha na kuondokana na umasikini,” alisema Gavana Prof.
Ndulu.
Aidha,
amesema kuwa Benki ya Dunia imesifu hatua zilizofikiwa na serikali ya
Tanzania katika kukuza na kusimamia uchumi wake ambao licha ya uchumi wa
dunia kushuka viwango vyake vya ukuaji uliotarajiwa wa asilimia 3.3 na
kukua kwa asilimia 1.5 tu, Uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi ya
asilimia 7.
“Tanzania
ni miongoni mwa nchi nne zinazoendelea ambazo uchumi wake unakua kwa
kasi na unatarajia kukua zaidi kutokana na kuvumbuliwa kwa gesi na
kushuka kwa mfumuko wa bei” Alisisitiza Prof Ndulu
Kiongozi
wa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo, Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa mkopo utakao tolewa ni pamoja na dola
milioni mia 2 kwaajili ya kulijengea uwezo shirika la ugavi wa umeme
nchini Tanzania-Tanesco ili liondokane na nakisi inayosababishwa na
madeni makubwa yanayolikabili shirika hilo
Dkt.
Mpango Amefafanua kuwa mkopo huo pia utaiwezesha serikali kulipa madeni
inayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii baada ya kufanyika kwa uhakiki
wa kina wa madeni hayo ili kuiwezesha mifuko hiyo itoe huduma
inayostahili kwa wananchama wake.
Amesema
kuwa kiasi kingine cha fedha hizo kitatumika kuijengea uwezo sekta
binafsi iweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Taifa pamoja na
kuimarisha kilimo kwa kuwawezesha wakulima kulima kilimo cha kibiashara
na kuondoa kodi zenye kuleta kero katika sekta ya kilimo.
“Wakati
tunatekeleza mpango huo tutaangalia pia namna ya kupitia upya kodi
zinazolalamikiwa katika sekta ya utalii” amefafanua Dkt. Mpango
Kwa
upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Dkt. Khalid Mohamed, ameishukuru Benki ya dunia kwa kuisaidia
nchi hiyo kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa visiwani
humo ikiwemo uboreshaji wa rasilimali watu, miundombinu ya barabara,
kiwanja cha ndege na kuboresha mazingira yatakayochangia kukua kwa sekta
ya utalii visiwani humo.
Makamu
wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Makhtar
Diop, amesema kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali ya
Tanzania ili iweze kufanikiwa kiuchumi na kijamii.
Amesifu
juhudi na hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya Tano
inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kwa kurejesha nidhamu ya kazi
na kupambana na vitendo vya ufisadi hatua ambayo inaungwa mkono na benki
yake ili kuharakisha maendeleo ya nchi na wananchi wake kwa ujumla.
Diop
amebainisha kuwa Benki yake inataka kuona Shirika la Umeme Tanzania
Tanesco linaboreshwa na kuwa la kisasa kwakuwa nishati ni nyenzo muhimu
ya kukuza uchumi wa viwanda na kwamba wangependa kusaidia eneo hilo
namengine ya kuboresha rasilimali watu kwa kuwekeza kwenye elimu na
kuwainua wananchi kimapato kupitia mradi wa TASAF na mingine
itakayoanzishwa.


No comments:
Post a Comment