
Hospitali ya rufaa ya Haydom
iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, imepatiwa msaada
wa mashuka 100 na benki ya CRDB ambayo yatatumiwa na wagonjwa wa
hospitali hiyo.
Akizungumza wakati akikabidhi
mashuka hayo 100 kwa mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk Emanuel Nuwass,
Meneja wa CRDB Tawi la Babati Ronald Paul alisema wanatoa msaada huo ili
kurudisha hisani kwa jamii.
Paul alisema wamekabidhi mashuka
hayo ili kutoa asante kwa jamii kwenye wiki ya huduma kwa wateja, kwa
kurudisha kwao kile kidogo wanachopata kwa ajili ya kuboresha mahusiano
zaidi baina ya benki hiyo na wateja wake.
“Tutaendelea kushirikiana na
kusaidiana kwenye masuala mbalimbali ya kijamii kwani tunatambua
jitihada na changamoto ya hospitali ya Haydom ambayo inatoa huduma kwa
watu wa Manyara na waliopo mikoa ya jirani,” alisema.
Hata hivyo, mkurugenzi wa
hospitali hiyo Dk Emanuel Nuwass alisema hii ni mara ya tatu kwa benki
hiyo kutoa msaada kwenye hospitali ya Haydom, hivyo iendelee kuwa karibu
nao kwa ajili ya kupeana ushirikiano wa kusaidia jamii.
Dk Nuwass alisema awali benki
hiyo ilitoa mchango wa maendeleo wa sh1 milioni kwa ajili ya siku ya
Haydom, kisha wakawapa zawadi ya ng’ombe mmoja mkubwa wa siku ya familia
na mashuka 100 yatakayotumiwa na wagonjwa.
Alisema hivi karibuni bodi ya
hospitali hiyo ilikubaliana na mpango wa malipo kwa wagonjwa kupitia
njia ya kadi ya CRDB na zoezi hilo linatarajia kuwarahisishia watu wote
watakaopata huduma katika eneo hilo la Haydom.
Kwa upande wake, meneja masoko
mwandamizi wa benki hiyo Fredrick Siwale alisema benki hiyo itandelea
kutoa huduma nzuri kwa wateja wao huku ikiboresha maeneo ambayo huduma
haipatikani kwa kuhakikisha wanakuwepo.
“Kupitia kauli mbiu yetu ya ulipo
tupo kama hatupo tutakuja na kama hatujaja utusubiri, tunalenga
kuwahudumia watanzania wote na kupitia hilo ndiyo sababu tukafika kutoa
mashuka haya kwani tunaithamini jamii,” alisema Siwale


No comments:
Post a Comment