
Katibu Mkuu Wizara ya
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Faustine Kamuzora akiwa na
mwakilishi kutoka Benki ya Dunia anaeshughulikia masuala ya Habari na
Mawasiliano Bi.Boutheina Guermazi wakati wa warsha ya Habari na
Mawasiliano ikizungumzia mafanikio ya mradi wa kuboresha miundombinu ya
Mawasiliano nchini na Serikali mtandao.
………………………………………………………
Na Daudi Manongi, MAELEZO.
Katibu Mkuu Wizara ya
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Faustine Kamuzora amesema kuwa
kata 345 zimefaidika na mradi wa kuboresha miundombinu ya mawasiliano
nchini na Serikali mtandao kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote.
Profesa Kamuzora amesema hayo
katika Warsha ya Habari na Mawasiliano iliyoandaliwa na Benki ya
Dunia ikishirikiana na Wizara hiyo ikizungumzia mafanikio ya mradi wa
kuboresha miundombinu ya Mawasiliano nchini na Serikali mtandao.
“Kupitia Serikali mtandao
tunataka huduma za serikali ziwafikie wananchi kokote walipo na
tunafahamu sasaivi wananchi wengi wana simu za mkononi na hivyo tunataka
huduma kama za manunuzi kama tenda za Serikali na usajili wa vizazi na
vifo kuanzia sasa zipatikane kwa njia ya mtandao ,huduma hii itaongeza
uwazi,ufanisi na ubora wa huduma katika shughuli mbalimbali za
Serikali.”Alisema Prof Kamuzora.
Pia Profesa Kamuzora amesema kuwa
Mradi huo ulilenga kufikisha mawasiliano vijijini na maeneo ambayo ni
magumu kufikika na wafanyabiashara na ilipata mkopo wa masharti nafuu wa
dola milioni 100 kutoka Benki ya Dunia ambao umesaidia kutoa ruzuku kwa
makampuni mbalimbali ya simu ili yaweze kujenga minara kwenye maeneo
ambayo hayana mvuto wa kibiashara na hivyo kufanikiwa kuwafikia wananchi
zaidi ya milioni 2.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka
Benki ya Dunia anaeshughulikia masuala ya Habari na Mawasiliano
Bi.Boutheina Guermazi amesema kuwa wataendelea kusaidia sekta ya
mawasiliano nchini kwa kuwa ni muhimu katika maendeleo ya nchi yeyote na
hivyo hawatasita kutoa misaada mbalimbali iwapo watahitajika kufanya
hivyo.
Akizungumzia mafanikio ya mradi
huo amesema kuwa kwa sasa kumekuwa na maboresho makubwa katika
mawasiliano na upatikanaji wa vifurushi vya intaneti kwani sasa vimekuwa
vya bei ya chini tofauti na mwanzo ambavyo vimesaidia upatikanaji wa
mawasiliano katika maendeleo ya nchi.


No comments:
Post a Comment