
FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti mwenza wa umoja wa Ukawa leo amemtuhumu Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa chama cha Wananchi (CUF), aliyerudishwa madarakani na Msajili wa Vyama Vya Siasa kwamba, amekuwa akifanya kafara kwenye Ofisi Kuu ya chama hicho, anaandika Charles William.
Mapema mchana wa leo katika tamko la viongozi wanaounda vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ilidaiwa kuwa Prof. Lipumba na wafuasi wake, wameigeuza Ofisi Kuu ya CUF Buguruni, jijini Dar es Salaam kuwa nyumba ya kulala wageni huku wakifanya vitendo vya kishirikina.“Viongozi wa Ukawa hatuwezi kuruhusu ofisi ya CUF kuwa ‘guest house’. Yule bwana na wenzake wanalala, wanaamka na kupiga mswaki katika ofisi za chama huku wakifanya vitendo vya kiganga kwa kuchinja kondoo na kuvunja nazi,” amesema Freeman Mbowe wakati akisoma tamko la Ukawa.
Akiwa ameambatana wenyeviti wengine watatu wa vyama vinavyounda Ukawa pamoja na makatibu wakuu wa vyama hivyo Mbowe alitoa tamko lililosainiwa na wenyeviti wa vyama vyote vya Ukawa.
“Yule bwana amekula cha mtu na kazi aliyopewa hajaimaliza, anataka kurejea ili amalizie kazi yake kwa kushirikiana na Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama Vya Siasa,” amesema.
Hata hivyo, Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, aliyerudishwa madarakani na Msajili wa Vyama Vya Siasa haraka amejibu kwamba, tuhuma hizo hazina msingi wowote.
“Wameishiwa hoja hao, sisi tupo ofisini hapa, wanaofanya vitendo vya kishirikina ni kina nani? wanaotoa madai hayo wanapaswa kuthibitisha ukweli wa madai yao,” amesema Kambaya.
Lipumba yuko kwenye mgogoro na Katibu Mkuu wake Maalimu Seif pamoja na kundi lake, Kambi ya Maali imemtimua uanachama Lipumba na Lipumba naye anasema kwamba hang'oki ng'o kwenye uongozi wa chama hicho hata iweje.
Anadai kwamba waliomtimua hawana mamlaka hayo kikatiba .
CHANZO;MWANAHALISI ONLINE


No comments:
Post a Comment