
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kulia) akimsikiliza
Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Nyanza (kulia), inayojenga barabara
ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50 mkoani Kigoma. Kushoto ni
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Kigoma Eng.
Narcis Choma.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiangalia nodo zinazoshikilia moja
ya madaraja yanayojengwa katika barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye
urefu wa KM 50 mkoani Kigoma.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoka kukaguzi wa moja ya
madaraja yanayojengwa kwenye barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu
wa KM 50 mkoani Kigoma.

Muonekano wa kalvati katika barabara ya Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50 mkoani Kigoma.

Muonekano wa barabara ya
Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50 mkoani Kigoma. Barabara hiyo kwa
sasa imefikia asilimia 18 ya ujenzi wake.
…………………………………………………………..
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameipa miezi minne Kampuni ya ujenzi
ya Nyanza Road Works kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara ya
Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 50 kukamilika kwa wakati na wananchi
wa Kibondo na maeneo ya jirani kuweza kuitumia.
Waziri Prof. Mbarawa ametoa kauli
hiyo wilayani Kakonko mkoani Kigoma mara baada ya kukagua barabara hiyo
na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake.
“Mwezi wa pili mwakani nitarudi
hapa kukagua tena maendeleo ya ujenzi wa barabara hii sababu bado kasi
mnayokwenda nayo hainiridhishi na kampuni hii ni ya kizalendo ambayo
ilitakiwa kuwa ya mfano”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa amemsisitiza
mkandarasi huyo kuzingatia viwango bora vya ujenzi wa barabara kama
ilivyosainiwa kwenye mkataba na kumtaka kuzingatia thamani ya fedha
katika ujenzi anaoufanya.
“Rafiki yangu ni yule anayefanya
kazi vizuri hata kama awe mwanangu kama hafanyi kazi vizuri
nitamfukuza”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Naye, Mkandarasi wa kampuni hiyo
Bw. Atul Ramji ameahidi kutii na kulifanyia kazi agizo la waziri huyo na
kusema kuwa ifikapo mwezi wa pili mwakani ujenzi utakuwa umepiga hatua
kubwa.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala
wa Barabara nchini (TANROADS),mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma amesema
ujenzi wa barabara hiyo kwa sasa umefika asilimia 18 kutoka asilimia
tano zilizokuwepo awali ambapo kwa sasa kazi zinazofanyika ni ujenzi wa
makalvati katika barabara hiyo.
Katika hatua nyingine Waziri
Mbarawa amemuagiza mkandarasi wa kampuni hiyo kuanza mara moja kuipatia
huduma ya maji Shule ya Sekondari ya Kanyonza angalau mara moja kwa wiki
kutoka kwenye kambi ya ujenzi wa barabara wakati Serikali ikiendelea
kutafuta suluhisho la kudumu.
Prof. Mbarawa amechukua hatua
hiyo baada ya wananchi wa kijiji cha Kanyonza kumsimamisha na kumueleza
changamoto ya Shule ya Sekondari hiyo iliyopo katika kijiji hicho
wilayani Kakonko kukabiliwa na uhaba wa maji hali inayowalazimu
wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya kilometa nne kufuata huduma hiyo


No comments:
Post a Comment