
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa uongozi wa
Wilaya ya Kibondo,alipotembelea ofisi hizo mkoani Kigoma.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akisikiliza taarifa kutoka kwa Mkuu wa
Wilaya ya Kasulu, Kanali Martin Mkisi mara baada ya kutembelea ofisi
hizo mkoani Kigoma.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa agizo kwa Wakala wa Barabara
nchini (TANROADS), kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wananchi
kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria madereva wote wa malori
ya mchanga na kokoto watakaobainika kutofuata sheria za ubebaji wa
bidhaa hiyo na hivyo kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo
mkoani Kigoma katika ziara yake ya kukagua barabara ya Kidahwe-Kasulu
yenye urefu wa kilometa 50 ambapo pamoja na mambo mengine amesema
Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu ya barabara kwa
maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla hivyo haita mvumilia mtu
yeyote atakayebainika kuharibu miundombu hiyo kwa makusudi.
“Kuanzia sasa Serikali
haitavumilia madereva wasiozingatia kanuni na sheria za usafirishaji wa
mizigo katika barabara nchini, hivyo nawaagiza Mameneja wa TANROADS
katika mikoa yote nchini kusimamia sheria ili kudhibiti miundombinu ya
barabara, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa ameliomba
Jeshi la Polisi kushirikiana vema na makandarasi wanaojenga miundombinu
ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini kuwakamata na kuwachukulia
hatua za kisheria baadhi ya watu wasio waaminifu ambao wanaiba vifaa vya
makandarasi jambo linalochangia kukwamisha shughuli za ujenzi wa
barabara.
Amewataka wananchi wa Wilaya ya
Kasulu kutoa ushirikiano kwa mkandarasi wa kampuni ya China Railway 15
Bureau Group Corporation anayejenga barabara hiyo ili kuwezesha ujenzi
huo kukamilika haraka.
Naye Meneja wa TANROADS mkoa wa
Kigoma Eng. Narcis Choma, amebainisha changamoto zinazokabili mradi huo
kuwa ni wizi wa mafuta na vifaa vya ujenzi hali inayosababisha mradi
kusuasua.
“Wananachi tambueni kuwa fedha
hizi ni za kwenu mnapohujumu vifaa vya ujenzi ni dhahiri
mnajicheleweshea maendeleo na kukwamisha fursa za kiuchumi katika wilaya
yenu”, amesema Eng. Choma.
Kwa upande wake Mhandisi Mkazi
Mekbib Tesfaye anayesimamia mradi huo kutoka Kampuni ya DOCH Limited,
amesema kuwa mradi huo umefikia asilimia 24 ambapo kwa sasa kazi
inayofanyika ni ujenzi wa madaraja mawili na makalvati katika barabara
hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri
Prof. Mbarawa ametembelea Chuo cha Mamlaka ya Hali ya Hewa Mkoani Kigoma
na kuahidi uongozi kuwa atazishughulikia haraka changamoto kadhaa
zinazokikabili chuo hicho ili kuweka mazingira rafiki ya kujisomea kwa
wanafunzi wanaosomea taalauma hiyo.


No comments:
Post a Comment