WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali tayari imeshalipa sh. bilioni 722.7 kati ya sh. bilioni 964.2
za madeni ya michango ya jumla ambayo Serikali inadaiwa na mifuko ya
hifadhi ya jamii nchini.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Oktoba
20, 2016) wakati akifungua Mkutano wa Sita wa wadau wa NSSF ulioanza leo
kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Arusha na
kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 600.
Amesema sekta hiyo imekua kwa asilimia 15
kutoka sh. trilioni 8.9 mwaka 2015 hadi kufikia sh. trilioni 10.2 mwaka
2016. “Hadi kufikia Juni 2016, takwimu zinaonesha idadi ya wanachama
imeongezeka na kufikia milioni 2.1. Rasilmali za mifuko zimefikia
shilingi trilioni 10.28 na mafao yaliyolipwa kwa kipindi cha mwaka
kinachoishia Juni 2016 ni shillingi trilioni 2.93. Michango ya wanachama
kwa mwaka ni shilingi trilioni 2.15 uwekezaji katika nyanja mbalimbali
umefikia kiasi cha shilingi trilioni 9.29,” ameongeza.
Waziri Mkuu pia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu
wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof. Godius Kahyarara
awaandikie barua waajiri wote wanaodaiwa na shirika hilo na kuwataka
wawasilishe fedha wanayodaiwa mara moja na wale ambao hawatalipa ndani
muda utakaowekwa wafikishwe mahakamani na yeye apewe taarifa.
“Kumekuwepo na changamoto ya muda mrefu ya
baadhi ya waajiri kutolipa michango kwa wakati hali inayoleta usumbufu
mkubwa kwa wanachama hasa wanapofikia muda wa kustaafu. Suala hili
halikubaliki, hivyo natoa maelekezo kwa waajiri wote nchini waheshimu
sheria na wawasilishe michango yao kwa wakati,” amesisitiza.
Mbali ya kuwabana waajiri, Waziri Mkuu pia
amewataka wanunuzi wa nyumba za shirika hilo na wapangaji wote
wanaodaiwa wakamilishe malipo yao na wasipofanya hivyo ndani ya muda
uliopangwa wafikishwe mahakamani.
“Nimeambiwa pia lipo tatizo la wadaiwa wa
nyumba yaani wanunuzi na wapangaji. Suala hili lilitolewa maelekezo na
Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu.
Nataka nisisitize kuwa watu wote walionunua nyumba za NSSF na bado
hawajakamilisha malipo na wale waliopanga lakini hawalipi kodi
wanatakiwa kulipa haraka au wakabidhi nyumba hizo kwa NSSF ziuzwe kwa
watu wengine, vinginevyo nao wafikishwe mahakamani.”
Akizungumzia utendaji wa shirika hilo,
Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa shirika hilo na Bodi ya Wadhamini
kwa uamuzi wake wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa sukari nchini. Amesema
kiwanda kitakachojengwa, kinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 100,000 kwa
Watanzania na hivyo kuongeza wanachama katika mfuko wa NSSF.
“Nimefurahishwa na uamuzi wa NSSF na PPF
kuungana ili kukabiliana na tatizo la sukari nchini. Tumeelezwa hapa
kuwa mashirika haya yatashirikiana kujenga Kiwanda cha Sukari
kitakachozalisha tani 200,000 kwa mwaka. Kiwanda hicho kitajengwa katika
eneo la Mkulazi lililopo mkoani Morogoro,” amesema.
Mapema, akielezea
utendaji wa shirika hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof. Godius
Kahyarara alisema limeboresha mafao ya wanachama wake kutoka sh. 80,000
hadi sh. 100,000 kwa mwezi.
Alisema limeanza kufanya upembuzi yakinifu
wa kujenga nyumba za watumishi Dodoma ili kuendana na uamuzi wa
serikali kuhamia Dodoma. “Upembuzi bado unaendelea lakini tumeshabaini
kuna uwezekano wa kujenga nyumba 200 hadi 300 mkoani Dodoma,” alisema.
Kuhusu uwekezaji kwenye ujenzi wa Daraja
la Mwalimu Nyerere lililopo Kigamboni, Dar es Salaam, Prof. Kahyarara
alisema uwekezaji huo unalipa kwa sababu makusanyo ya tozo kwa watumiaji
yamefikia asilimia 109. “Tuna uhakika kwamba fedha tulizowekeza
zitarudi,” amesisitiza.
Wakati huohuo, Waziri
Mkuu amepokea msaada wa tani 45 za saruji ambazo ni sawa na mifuko 900
yenye thamani ya sh. milioni 15 kwa ajili ya waathirika wa tetememo la
ardhi mkoani Kagera. Amepokea msaada huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi
ya Wadhamini ya NSSF, Prof. Samuel Wangwe.
Akiwasilisha msaada huo, Prof. Wangwe
alisema wameguswa na tatizo lilitokea mkoani Kagera na wameamua kutoa
mchango ili kusaidia juhudi za Serikali kukabiliana na maafa hayo. Pia
alisema wamekamilisha ahadi yao ya madawati 6,000 yenye thamani ya sh.
milioni 400 ambayo waliitoa awali.
Waziri Mkuu aliwashukuru kwa misaada hiyo na kuwahakikishia kwamba itafikishwa kwa walengwa



No comments:
Post a Comment