Halmashauri ya Jiji la Arusha
inakanusha taarifa ya uzushi na upotoshaji iliyosambazwa kwenye mitandao
ya kijamii jioni ya leo tarehe 17.10.2016 ikimuhusisha Mkurugenzi wa
Jiji la Arusha Ndg. Athumani Kihamia pamoja na Mbunge wa Viti Maalum
Mkoa wa Arusha Mhe. Catherine Magige.
Taarifa hiyo ya kughushi
iliyochapishwa kwa kutumia nembo ya Jiji la Arusha imetengenezwa na watu
wenye nia ovu na dhamira mbaya kwa malengo ya kupunguza kasi ya
utendaji wa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Ndg. Athumani Kihamia pamoja
na Serikali Mkoani Arusha kwa ujumla.
Aidha taarifa hiyo ya uzushi
imebeba ujumbe wa kutunga wenye kusudio maalum la kumchonganisha
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha na mamlaka nyingine ikiwemo Mamlaka yake ya
Uteuzi ili kumchafulia jina na kumgombanisha na Mamlaka hiyo.
Halmashauri ya Jiji la Arusha
inaziomba Mamlaka zinazohusika na ufuatiliaji wa uhalifu wa mitandao
zikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) na Jeshi la Polisi Nchini
kufuatilia watu wote walioshiriki upotoshaji na uhalifu huo wa
kimtandao na kughushi ili kuwatia nguvuni na kuwachukulia hatua kali za
Kisheria ili iwe fundisho kwao na watu wengine wenye tabia ya aina hiyo.
Hata hivyo Halmashauri ya Jiji la
Arusha inapenda kuujulisha Umma kuwa, Mkurugenzi wa Jiji ataendelea
kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na kanuni zilizopo kusimamia maslahi ya
Umma, kudhibiti mapato na matumizi ya Fedha za Umma ili kuhakikisha
maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutaka Fedha nyingi zitumike
kwa ajili ya shughuli za maendeleo na hasa kuwahudumia wanyonge
inatekelezwa ipasavyo. Pia Halmashauri ya Jiji inatoa wito kwa wadau
wote ndani ya Jiji la Arusha kuunga mkono jitihada hizo za kuwahudumia
wanyonge.
Halmashauri ya Jiji inapenda
kuwaarifu watanzania wote kuipuuza mitandao inayotoa habari za uzushi na
kupuuza habari hiyo na nyinginezo za uzushi zinazoenezwa dhidi ya
viongozi kwani hazina ukweli wowote zaidi ya uchochezi na uchonganishi.
Aidha Halmashauri ya Jiji la
Arusha inawashauri wahusika wote wa uzushi huu kuacha kupoteza muda
badala yake waungane na Serikali katika utekelezaji wa Kauli Mbiu ya
HAPA KAZI TU.
Nteghenjwa Hosseah
Afisa Habari, Halmashauri ya Jiji
Arusha.
17 Oktoba,2016



No comments:
Post a Comment